RUKWA YAZINDUA DAWATI LA UWEZESHAJI BIASHARA
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuzindua dawati maalum la uwezeshaji biashara, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma kwa wafanyabiashara, hususan wadogo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RC Makongoro amesema dawati hilo litasaidia kusikiliza changamoto, kutoa elimu ya kodi na kuondoa vikwazo vya kibiashara, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa.
Aidha, Mheshimiwa Makongoro ametambua na kupongeza mafanikio ya TRA katika makusanyo ya mapato kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na kuendelea kufanya vizuri katika miezi ya Julai na Agosti 2025/2026. Ametoa shukrani kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Mwenda, kwa maono ya kuanzisha dawati hilo kitaifa, lililozinduliwa Agosti 16, 2025, mkoani Morogoro.
Kwa Mkoa wa Rukwa, dawati hilo litapatikana katika wilaya za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo na kituo cha huduma kwa mlipa kodi Laela.
RC Makongoro amewataka wafanyabiashara kulitumia dawati hilo kwa ushirikiano na si kwa hofu, huku akiahidi ushirikiano wa Serikali ya Mkoa na taasisi mbalimbali ili kuifanya Rukwa kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji.
Mwisho, amewashukuru viongozi wa wafanyabiashara kwa ushirikiano wao na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha wadau katika maamuzi ya kikodi ili kujenga misingi ya uwazi na haki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa