Na Khadija Dalasia - Rukwa,
Baraza la Biashara Mkoa wa Rukwa limefanya kikao chake 22 Oktoba 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kikiwahusisha wafanyabiashara mbalimbali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mheshimiwa amesisitiza dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha mazingira ya biashara na kuleta maendeleo kwa watanzania.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ameeleza umuhimu wa majadiliano yenye tija kati ya sekta binafsi na Serikali ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Mheshimiwa Chirukile amesema sekta binafsi ni injini ya uchumi, hivyo ni muhimu kutengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara ili waendelee kukuza biashara zao na kulipa kodi inayosaidia kugharamia miradi ya maendeleo.
Maboresho ya miundombinu ya uwanja wa ndege, ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika, na ujenzi wa barabara ya Matai hadi Kasesya na Ntendo-Muze-Kilyamatundu. Mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha inaendelea kuweka mazingira yatakayowavutia wawekezaji kuwekeza Mkoani Rukwa na kuimarisha sekta binafsi.
Mkuu wa Wilaya amezungumzia maboresho ya kimfumo yaliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanayoruhusu wafanyabiashara kuomba namba ya udhibiti (Control Number) na TIN bila kufika ofisini na kuanzishwa kwa Kituo Kodi katika eneo la Laela ili kufikia vijiji kama Kilyamatundu, Mtowisa, Muze, Kaengesa, na Mpui kama sehemu ya jitihada za kuboresha mazingira ya kibishara Mkoani Rukwa.
Kikao hicho ni mwendelezo wa jitihada za Serikali ya Mkoa wa Rukwa katika kuboresha mazingira ya biashara, huku ikishirikiana kwa karibu na sekta binafsi ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Chirukile amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa katika kikao hicho. Mkuu wa Mkoa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa