Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Rukwa
Serikali imetangaza dhamira yake ya kuwalipa wakulima 156 wa mahindi jumla ya Shilingi 315,118,510 kutokana na kuzulumiwa na mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Ndg. Linus Kalandamwazye.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ametoa kauli hiyo jana tarehe 13 Octoba 2019 wakati akizungumza na wanachama wa Muzia Amcos Wilayani Kalambo wakati akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Rukwa.
Malipo hayo yatawahusu wakulima wa Tarafa ya Mwimbi yenye kata nne ambazo ni Mambwe Kenya, Ulumi, Mkombo na Mwazye kutokana na kupima mahindi yao zaidi ya Tani 622.679 kwenye Chama cha Muzia Amcos kilichopewa uwakala na serikali wa kununua mazao kwa wakulima tarehe 8 Agosti 2017 kwa makubaliano ya kulipwa ndani ya wiki tatu kutoka tarehe ya kupimwa lakini hawakulipwa mpaka sasa.
“Kesi ikiwa mahakamani serikali haiwezi kuingilia badala yake wakati tunaendelea na kesi hiyo ninaziagiza taasisi zangu tatu kuchanga fedha kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao” Alikaririwa Mhe Hasunga
Alisema wanaotakiwa kuchanga fedha hizo kwanza ni Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kulishughulikia jambo hilo kwa wakati ili wakulima hao waweze kulipwa fedha zao.
Ameiagiza pia Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuchanga fedha hizo kwani wao ndio wasimamizi wa Vyama vya Ushirika lakini kwa kipindi chote wameshindwa kushughulikia changamoto hiyo ya wakulima.
Kadhalika, Mhe Hasunga Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuchangia fedha hizo.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli haina dhamira ya kuwadunisha na kuwafedhehesha wananchi badala yake imejipambanua kuwanufaisha wakulima katika kilimo.
Alisema kuwa serikali imeamua kuwalipa fedha hizo wakulima ili kuendelea na uzalishaji bora wa mazao ya kilimo lakini kesi itakapomalizika serikali itazidai fedha hizo.
Mhe Hasunga amemuagiza Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Rukwa kupanga vizuri madai ya wakulima hao huku akisisitiza kutoingizwa majina mapya (Majina Hewa) yasiyohusika na madai ya fedha hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe Joachim Wangabo amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) kwa kukubali kulivalia njuga jambo hilo kwa kuwalipa fedha hizo wakulima kwani kufanya hivyo kutarahisisha wakulima hao kuendelea na uzalishaji wa mazao katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020.
Amesema kuwa maamuzi hayo ya wizara kuamua kuwalipa wakulima huku taratibu zingine za kisheria ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa hatua Mwenyekiti huyo zikiwa zinaendelea zimeibua ari na nguvu mpya katika kilimo.
Awali, akisoma taarifa ya malalamiko ya kutapeliwa fedha hizo katibu wa chama cha MUZIA AMCOS Ndg Geofrey Mbati amesema kuwa pamoja na kupeleka malalamiko katika maeneo mengi lakini ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwa ushirikiano wa karibu katika kipindi chote cha kutafuta muarobaini wa malipo ya wakulima.
Alisema kuwa miongoni mwa maoni ya wakulima ilikuwa ni ombi la kupatiwa fedha hizo kwa ajili ya kuwanusuru kutokana na kadhia hiyo ya muda mrefu iliyopelekea kushindwa kulipa ada za wanafunzi shuleni, kushindwa kuwekeza tena kwenye kilimo pamoja na kushindwa kumudu gharama za maisha hali iliyopelekea kuishi maisha ya kifukara.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa