Kalambo, Rukwa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepiga marufuku kwa watumishi wa umma kuwaomba au kupokea malipo yoyote kutoka kwa wafugaji kwa ajili ya huduma za chanjo na utambuzi wa mifugo, ikiweka bayana kuwa huduma hizo zinatolewa bure kwa ufadhili wa Serikali.
Akizungumza Julai 8, 2025, katika Ranchi ya Taifa ya Kalambo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Edwin Mhede, alisema Serikali inalipa gharama zote za utekelezaji wa zoezi hilo kwa asilimia 100, na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka agizo hilo.
"Zoezi hili ni la kitaifa, linaendeshwa kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alilizindua rasmi tarehe 16 Juni, 2025 huko Simiyu. Hakuna mfugaji anayepaswa kutozwa hata shilingi moja. Serikali inalipia kila kitu," alisema Dkt. Mhede.
Dkt. Mhede alibainisha kuwa katika mikoa ya Rukwa hususan wilaya za Nkasi na Kalambo, zoezi hilo linaendelea na tayari zaidi ya ng’ombe 1,500 kati ya zaidi ya 36,000 waliolengwa, wamekwishachanwa na kutambuliwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Ndugu Robert Msalika Makungu, alieleza kuwa mkoa huo unatarajia kuchanja zaidi ya ng’ombe 400,000 pamoja na mbuzi, kondoo na kuku, huku akisisitiza kuwa utaratibu wa ufuatiliaji umewekwa ili kuhakikisha utekelezaji unafanyika kwa haki, uwazi na ufanisi.
Baadhi ya wafugaji waliopatiwa huduma hiyo akiwemo Bi. Mgaya Myende wa kijiji cha Nkana na Bw. Benueli Makselo wa Sintali, walisema wamefurahishwa na zoezi hilo ambalo wamedai linapunguza gharama za matibabu ya mifugo, kuboresha afya ya wanyama wao, na kuongeza ulinzi kupitia heleni za utambuzi zinazotolewa bila malipo.
Zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha usimamizi wa mifugo nchini, kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya mifugo, pamoja na kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga maendeleo ya sekta hiyo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa