Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imekabidhi pikipiki nane (8) kwa Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Makabidhiano ya pikipiki hizo yamefanywa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Felister Peter Mdemu.
Bi. Mdemu amebainisha kuwa pikipiki hizo ni nyenzo muhimu za kazi zitakazorahisisha mawasiliano na ufuatiliaji wa shughuli za maendeleo katika maeneo ya vijijini na Kata. Amesema kuwa Serikali imekusudia kuongeza ufanisi wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya maendeleo, kuimarisha ushiriki wa jamii katika miradi ya kijamii, na kuchochea uwajibikaji katika ngazi za chini za utawala.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Daudi Sebyiga, amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa imeboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri za Mkoa wa Rukwa. Amesisitiza kuwa pikipiki hizo zitaongeza kasi ya utoaji huduma na kufikisha elimu ya maendeleo kwa wananchi kwa wakati.
Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopokea pikipiki hizo wameishukuru Serikali ya kwa kuwapatia vyombo hivyo vya usafiri, wakibainisha kuwa vitasaidia kupunguza changamoto ya usafiri na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika maeneo ya vijijini.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo Oktoba 24, 2025 mkoani Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa