Serikali Mkoani Rukwa kwa kushirikiana na Kiwanda cha Alpha Tanganyika Flavour Ltd imezindua siku ya Uhamasishaji wa kula Samaki mkoani humo kwa lengo la kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya mchanganyiko wa vyakula vya makundi tofauti yanayozalishwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huku msisitizo ukitolewa katika ulaji wa samaki.
Tafiti zinaonesha kuwa hali ya udumavu na utapiamlo kwa Watoto walio na umri chini ya miaka mitano mkoani humo imeshuka kutoka asilimia 56.3 ya mwaka 2016 hadi asilimia 47.9 ikiwa ni kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na mkoa katika kupambana na hali hiyo ambayo inasababishwa na na ulaji wa chakula cha aina moja hasa kundi la chakula cha wanga kuliko makundi mengine ya vyakula hasa protini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati wa uzinduzi wa siku hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amesema kuwa Mkoa wa Rukwa una vyanzo vingi vya uzalishaji wa samaki ikiwemo Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa, Bwawa la Sundu, Bwawa la Kwela Pamoja na mabwawa 328 yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya mkoa.
Aidha, Alisema kuwa kwa mwaka 2018/2019 na 2019/2020 wastani wat ani 2,444.323 za samaki zimevuliwa katika vyanzo hivyo vya uvuvi na kuongeza kuwa asilimia 15 hadi 30 ya mwili wa samaki ni protini na mafuta ya samaki yana Omega 3 kuonyesha kuwa ni mafuta bora na salama katika mwili wa binadamu kwani hayasababishi magonjwa ya moyo kama yalivyo mafuta mengine.
“Ndugu Washiriki sisi kama serikali tutaendelea kushirikiana na mwekezaji Alpha Tanganyika Flavor Ltd katika kuhakikisha kuwa tunawahamasisha wananchi wa mkoa wa Rukwa kula Samaki ili wawe na soko namba moja la kiwanda cha Alpha Tanganyika kwenye mkoa wetu wa Rukwa, nikuhimize mchakate samaki kwa ubora wa kiwango kinachohitajika katika soko la ndani na nje ya mkoa n ahata nje ya nchi ili uutangaze mkoa wetu kupitia zao hili la samaki,” Alisema.
Amezungumza hay oleo tarehe 19.12.2020 wakati wa hafla ya uzinduzi wa siku ya uhamasishaji wa ulaji samaki mkoani Rukwa shughuli iliyohudhuriwa na uongozi wa wavuvi wa Samaki mkoa wa Rukwa, Maafisa Uvuvi wa halmshauri na Mkoa, Pamoja na wadau wengine wa zao la Samaki.
Wakati akisoma risala, kwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Alpha Tanganyika Flavor Aplha Nondo alisema kuwa Pamoja na malengo mengine ya kuanzisha kiwanda hicho lakini lengo kuu ni kuwatapatia wavuvi wa Ziwa Tanganyika soko la uhakika na hivyo kusababisha kutotumia musda mrefu kusafirisha samaki wao kwenda nchi ya jirani ya Zambia namatokeo yake kukosa muda wa kukaa na familia zao.
“Tuko hapa kufanya mambo yafuatayo, kwanza kuawapa wavuvi wa ziwa Tanganyika uhakika wa soko, tunaamini tukifanya hivyo kwanza wake wa wavuvi tunawarudishia waume zao, ule muda ambao walikuwa wanatumia baada ya siku nzima yuko kwenye maji masaa manne kwenda Zambia ule muda watarudi nyumbani watakaa na wake zao, ule muda watarudi nyumbani watakaa na Watoto wao, wale ambao Watoto wao hawakuwa wakiwaona wataanza kuwaona, labda Watoto wa wengine walikuwa wanauliza baba anakaa Zambia ama Tanzania, watajua kwamba baba ni Mtanzania na anakaa Tanzania,” Alisema.
Akiongea kwa niada ya wadau wa wavuvi wa samaki Diwani wa Kata ya Kabwe, Wilayani Nkasi Mh. Asante Lubinsha aliushukuru uongozi wa Kiwanda cha Alpha Tanganyika Flavor Ltd, kwa kufungua kiwanda cha Samaki mkoani humo akiamini kuwa kitakuwa ni tegemeo kubwa kwa wavuvi na kutarajia kuwatoa katika hali ya umasiki na kuwasababisha kuwa katika hali ya kati nakati.
“Sisi kama wavuvi, tunategemea sana kiwanda hiki ktatukomboa kiuchumi na tumekuwa tukihangaika sana kuongea na wabunge wetu ili watutafutie wawekezaji ambao tukimtumia vizuri sisi wavuvi itakuwa ni eneo la ukombozi wetu, ukiangalia Mwanza kuna viwanda vya kutosha, Dar es Salaam kuna viwanda lakini mkoa wetu bado uko nyuma katika suala zima la viwanda,” Alisema.
Kwa takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi za mwaka 2019/2020 zinaonyesha ulaji wa samaki kwa Mtanzania mmoja ni Kilo 7- 8 kwa mwaka, Kiasi ambacho ni kidogo ukulinganisha na maelekezo ya FAO Shirika la chakula Duniani ambapo mahitaji ya mtu mmoja kwa mwaka ni kilo 21 huku watanzania milioni 6 wakitegemea kipato chao kutokana na Samaki wanaovuliwa tani zaidi ya 300,000 kwa mwaka nchini huku sekta ya uvuvi ikichangia asilimia 1.7 kwenye pato la taifa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa