Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kuhakikisha anatatua changamoto chache zilizobaki katika umaliziaji wa Stendi kuu ya Mabasi Katumba Azimio mjini Sumbawanga kabla ya kuifungua kwa majaribio ifikapo tarehe 5.2.2021.
Pamoja na hayo Mh. Wangabo amesema kuwa ili kuepuka migogoro ya kisheria amemtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha anafanya kikao na wadau wa stendi hiyo ikiwemo mkandarasi Pamoja na mshauri elekezi wa mradi huo kabla ya kuruhusu kuanza kutumika kwa stendi hiyo ambayo ilitakiwa kumalizika mwezi Septemba mwaka 2020.
Aidha, Mh. Wangabo ametaja maeneo kadhaa ikiwemo mifumo ya maji ambayo itasaidia matumizi rahisi ya vyoo ambayo bado haijakamilika ipasavyo na hivyo kumuelekeza mkurugenzi huyo kurijiridha na ufanyaji kazi wa mifumo hiyo kabla ya kufunguliwa kwa stendi.
“Wahusika wote Make, mjiridhishe wote masuala ya kisheria lakini pia haya maeneo muhimu haya, ambayo niliyasema muwe mmeyashughulikia vizuri, haitapendeza kuona watu wanajazana hapa halafu vyoo havifanyi kazi, lakini pia upande wa wadau mbalimbali ni lazima mkae nao, msikilize hata maoni yao halafu ndio muanze, haipendezi kuanza na migomo, unakuja huku unasikia mgomo, kwahiyo kabla ya kuanza mjiridhishe vizuri, kesho keshokutwa watu wataanza kusema mmefungua haraka haraka, hatutaki migomo tunataka watu wafanye shughuli kwa utulivu,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo ameyasema hayo 28.1.2021 alipotembelea kituo hicho kikuu cha mabasi kilichopo Katumba Azimio, manispaa ya Sumbawanga kwaajili ya kukikagua kabla ya kufnguliwa kwake akiwa Pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Halikadhalika katika kufanya maandalizi ya ufunguzi wa stendi hiyo Mh. Wangabo amewataka kuchukua tadhari ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu Covid-19 kwa kuweka sehemu za kunawia Pamoja na tahadhari nyingine za kiusalama.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya akiongea kabla ya maelekezo hayo ya mkuu wa mkoa alisema kuwa awali Stendi hiyo ilikuwa ifunguliwe tarehe 15.1.2021 lakini haikufanikiwa na hivyo kusogeza mbele hadi tarehe 29.1.2021 wakisubiri Mshauri Elekezi aweze kuruhusu wakati shughuli nyingine zikiendelea kukamilishwa na kuongeza kuwa Manispaa bado inaendelea kuomba fedha hazina ili kuweza kukamilisha mradi huo.
Akitoa maoni yake Mkandarasi wa mradi huo Mkurugenzi wa Kampuni ya Sumry Enterprises Humud Sumry ameuomba uongozi wa mkoa wa Rukwa kubainisha kuwa Pamoja na kufunguliwa kwa stendi hiyo ya Mabasi lakini kuna vikao vya wadau wa mradi huo havijakaliwa ili kuyaweka mambo sawa na hatimae kuzuia sintofahamu baada ya kufunguliwa kwa stendi hiyo.
Wakati akitoa taarifa ya ujezi wa Stendi hiyo Kaimu Afisa Mipango wa manispaa ya Sumbawanga Ardius Kwimba alisema kuwa kwa ujumla ujenzia wa stendi hiyo umekamilika kwa asilimia 95 na kazi nyingine zikiendelea kwenye maeneo tofauti kulingana na mkataba.
“Kuweka matofali yaani ‘pave blocks’ kwenye eneo la kuegeshea mabasi yaendayo mikoani, mabasi yaendayo vijijini, bajaji, bodaboda, teksi na baiskeli kazi imefanyika kwa 100%, ujenzi wa vyumba vya maduka 10 umefanyika kwa 100%, jengo la utawala ghorofa moja umefanyika kwa 95%, kituo cha polisi kwa 97%, Choo cha kulipia kwa 97%, Ujenzi wa uzio wa mageti matatu kwa 75%, vyumba vya ATM kwa 97%, Gym kwa 97%, Kibanda cha mlinzi kwa 80%, mfumo wa mifereji ya mvua kwa 95%, mfumo wa umeme kwa 55%, halmashauri imeweka mfumo wa maji ili kituo kianze kutumika,”Alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa