Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Rukwa imetakiwa kufanya uchunguzi wa manunuzi yote ya vifaa vya ujenzi yaliyofanyika katika miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa kipindi cha Mwaka 2021/2022.
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 16 Juni 2023 na Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kupokea na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2021/2022.
Katika taarifa hiyo ambayo imeonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imepata hati yenye mashaka, mapungufu yaliyobainishwa na Mkaguzi ni maeneo ya uandaaji wa taarifa za hesabu za Halmashauri, malipo yaliyokosa viambata na yenye viambata visivyo sahihi.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuwachukulia hatua stahiki watumishi wote ambao wameisababishia Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi hoja zilizopelekea Halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kufanya kazi kwa ushirikiano na kusisitiza kila mtumishi kutimiza wajibu wake.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa