RC MKIRIKITI: BILIONI 12 KUTEKELEZA MIRADI YA TARURA.
Wakandarasi wanaofanya kazi ya kutekeleza miradi chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye mkoa wa Rukwa wametakiwa kuzingatia nidhamu ya kazi ili miradi iwe bora na endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa agizo hilo leo (01.11.2021) wakati wa kikao cha kazi na wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali chini ya Tarura kwa mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
Mkirikiti ameonya tabia iliyoanza kujengeka miongoni mwa wakandarasi kuona miradi hiyo siyo ya kipaumbele wakati inatumia fedha nyingi za walipakodi wa Tanzania.
“Nidhamu kwenye utendaji kazi wa wakandarasi ni jambo muhimu ili fedha zinazotolewa na serikali kupitia TARURA zitumike kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya ya ubora wa miradi ya barabara zetu. Nataka kuona mkoa huu wakandarasi mnaheshimu mikataba yenu ya kazi,” alisisitiza Mkirikiti.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni kikao chake cha kwanza na wakandarasi wa miradi ya barabara aliwafahamisha kuwa tayari serikali imekwisha toa shilingi Bilioni 12 kwa ajili miradi 49 kote kwenye halmashauri chini ya Tarura katika kipindi cha mwaka huu.
Mkirikiti alitumia pia kikao hicho kutoa onyo kwa wahandisi wa TARURA kwenye halmashauri za mkoa wa Rukwa kuacha tabia ya kutoa kazi kwa wakandarasi wasio na sifa na uwezo wa kutekeleza miradi hatua inayorudisha nyuma jitihada za serikali.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa Mhandisi Seth Mwakyembe alisema katika kikao hicho jumla ya mikataba ya ujenzi 16 yenye thamani ya shilingi Bilioni 4.5 ikiwa ni sehemu ya Shilingi Bilioni 12 itasainiwa baada ya uchambuzi wa kina kujiridhisha na sifa za wakandarasi.
Mwakyembe alimfahamisha Mkuu wa Mkoa kuwa, Tarura imejipanga kuhakikisha miradi hii itakayosainiwa licha ya kuwa ni kipindi cha mvua kukaribia itakwenda kutekelezwa kwa kasi na kwa ubora ili kutatua changamoto za barabara hususan vijijini.
“Tarura inatoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa kuboresha barabara za mjini na vijijini ambako watanzania wana uhitaji wa miundombinu bora. Tutasimia fedha hizi zilete tija” alisema Mhandisi Mwakyembe.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya JEMO Mary Obadia Mbwilo akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wa Rukwa alisema anaishukuru serikali kwa kutoa kipaumbele cha kazi kwa wakandarasi wa Rukwa wakiwemo wanawake hatua inayosaidia wakuze uwezo wao wa kazi na uchumi.
Mdau huyo alibainisha kuwa “tupo wakandarasi wanawake wanne(4) tuliopata kazi msimu huu, hatutawaangusha tutatekeleza kazi kwa ubora ili siku za mbele wanawake zaidi wenye ujuzi na uwezo waweze kupata mikataba ya kazi TARURA” alihitimisha Mbwilo.
Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa Daniel Ntera akitoa mada kwa wakandarasi hao amewataka wazingatie mikataba yao ya kazi na kutojishusisha na vitendo vitakavyohujumu ubora wa miradi.
Ntera aliwafahamisha kuwa Takukuru inafuatilia kwa karibu kazi zote za wakandarasi ili kudhibiti mianya ya rushwa hatua itakayosaidia miradi iwe bora na fedha za umma zitumike kwa kazi zilizopangwa kwenye mikataba.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa