TASAF IFUNDISHE STADI ZA KUKUZA KIPATO - RC SENDIGA
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ameagiza wataalam wanaosimamia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika ngazi ya halmashauri kuwafundisha wanufaika stadi za kazi zitakazosaidia kuinua kipato cha wananchi.
Ametoa kauli hiyo ( Februari 04,2023) wakati kukagua kikundi cha wanufaika wa TASAF waliopo kijiji cha Ilemba Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga wanaojishughulisha na mradi wa miti ya matunda na mbao.
“Wafundisheni wanufaika hawa kuwa na miradi yao ya mashamba ya miti au ufugaji mifugo katika kaya zao ili kipato kidogo wakipatacho toka serikalini kiwe ni mtaji wa kukuza uchumi . Wafikirie kubuni miradi siyo kutegemea fedha za TASAF” alisema Sendiga.
Sendiga aliongeza kusema fedha wanazopata wanufaika siyo fungu la mirathi na kuwa wasipewe kama sadaka bali wafundishwe ujasiliamali wa kuwa na miradi yao ili siku serikali ikisitisha programu hiyo waweze kujitegemea.
Nao wanufaika wa TASAF toka kijiji cha Ilemba waliozungumza na mwandishi wetu walikuwa na haya ya kusema ,Everada Kapaya alisema amenufaika na mfuko wa Tasaf tangu mwaka 2015 ambapo ameweza kujenga nyumba ya vyumba viwili na kusomesha watoto wake wanne pamoja na kuanzisha ufugaji wa ng’ombe mmoja .
Evarada alisema ‘nashukuru serikali kwa mradi huu wa Tasaf na ninaomba Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kutusaidia ili tuweze kusomesha watoto wapate elimu nzuri” .
Naye Elizabeth Pesambili mkazi wa Ilemba alisema kupitia mfuko wa Tasaf ameweza kulea wajukuu zake 16 ambao aliachiwa na watoto wake na kuwa sasa ana miaka mitano akipata pesa toka serikalini.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo wa Rukwa alikagua miradi ya ujenzi wa zahanati kijiji cha Muze, Uzia, Hospitali ya Wilaya Mtowisa pamoja na shule za sekondari Mazoka na Ilemba .
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Jane Nyamsenda akizungumza kwenye ziara hiyo alisema atahakikisha anashirikiana na wananchi wa Sumbawanga kutekeleza miradi yote iliyopo na kubuni mingine kwa ustawi wa jamii.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa