Wadau mbalimbali wa michezo katika mji wa Sumbwanga wamejitokeza kwa wingi kuipa mapokezi ya aina yake timu ya jeshi la Magereza Tanzania – Tanzania Prisons ambayo imethibitisha kuutumia uwanja wa Nelson Mandela Mkoani Rukwa kama uwanja wake wa nyumbani katika msimu wa 2020/2021 wa Ligi Kuu Bara jambo ambalo lilikuwa likisubiriwa kwa hamu na wananchi wa mkoa huo ili kupata burudani ya michezo waliyoikosa kwa zaidi ya miaka 23.
Juhudi hizo za kufanikisha timu hiyo kuweka makazi yake katika mkoa huo ni ushawishi mkubwa uliofanywa na mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo pamoja na uongozi wa mkoa huo huku akiungwa mkono na wadau wa michezo mkoani humo baada ya kuona faida kubwa iliyopatikana kutokana baada ya fainali za kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kufanyika katika uwanja huo uliokarabatiwa kwa kiwango cha hali ya juu.
Wakati akizungumza baada ya kamanda wa Jeshi la magereza mkoa wa Mbeya kuikabidhi timu hiyo kwa kamanda wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Rukwa Mh. Wangabo alisema kuwa ndoto waliyokuwa wakiiota sasa imegeuka kweli baada ya timu hiyo kutua rasmi katika mkoa na wananchi kuishuhudia ikiingia katika uwanja wa Nelson Mandela ambao utatumika katika mechi zao za Ligi Kuu.
“Timu hii imekuja wakati muafaka, tumekuwa hatuna timu katika ligi daraja la kwanza, daraja la pili, mpaka huko ligi kuu hatuna kwa miaka mingi sana, zaidi ya robo karne, hatuna timu kwahiyo na wananchi wamekosa burudani hii, na hawa watu wote hawa unaowaona hapa wamekuja wanapenda michezo, sisi tulikuwa tuna deni kubwa kama viongozi, tunaongoza wananchi ambao tunawanyima furaha, sasa tumeamua kuwapa furaha wanarukwa wote pamoja na wa mikoa ya jirani,” alisema.
Aidha, Ameiombea timu hiyo kushinda michezo yake yote miwili ya ugenini ambayo wanaanza na timu ya Young Africans SC pamoja na KMC FC katika jiji la Dar es salaam na kufuatiwa na mechi za za Nyumbani wataanza na Namungo FC, Azam FC pamoja na Simba SC zitakazochezwa katika Uwanja huo wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga.
“Mwezi wa kumi tunacheza na Simba SC ya Dar es Salaam, sasa siku hiyo, nilisema hizi timu nyingine zisione zitafute mpira kwa tochi, hawa Simba ndio wasiuone kabisaaa, mpaka waulize hivi goli liko wapi, pengine goli liwe hili benchi la ufundi, yaani nasema wasione mpira kwa namna mtakavyotandaza mpira hapa, pasi fupi fupi na ndefu muwachanganye kabisa mpaka wapoteane hapa,” Alisisitiza.
Katika mapokezi hayo MH. Wangabo aliikabidhi timu hiyo Seti ya jezi pamoja na mipira kwaajili ya maandalizi yao kuelekea kuanza kwa ligi hiyo tarehe 6.8.2020 huku kamati maalum inayoshughulikia ustawi wa wachezaji wa timu hiyo ikiongozwa na Mzee Dkt. Chrisant Majiyatanga Mzindakaya wakitoa chakula kwa wachezaji pamoja na ng’ombe mmoja
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa