Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa David Kilonzo amewaonya watumishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa kutosuburi misaada kutoka nje ndipo wayafanyie kazi masuala ya UKIMWI na badala yake wayasimamie na kuyajadili kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo.
Amesema kuwa Suala la UKIMWI ni lazima lichukuliwe hatua na watanzania wenyewe kama waathirika wakuu na kama tutaendelea kusubiri misaada ndipo tujadiliane na kushughulikia masuala ya UKIMWI basi vifo vitaongezeka.
“Misaada kutoka nje haiwezi ikatufanya tukabadilika, tunatakiwa sisi wenyewe kila mara kupata muda wa kujadili kuhusu suala la UKIMWI kwasababu UKIMWI upo pamoja na sisi, UKIMWI hauchagui Idara wala Taasisi, hivyo hatuna budi kuendelea kujikinga na kuhamasisha wengine wajikinge,” Alisema
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa kwa watumishi wa sekretarieti ya Mkoa wa Rukwa chini ya udhamini wa shirika la Walter reed.
Kwa Upande wake mratibu wa TACAIDS Mkoa wa Rukwa Daniel Mwaiteleke amesema kuwa kwa Mkoa wa Rukwa maambuki ya UKIMWI yamepungua kutoka 6.2% mwaka 2012 hadi kufikia 4.4% kwa mwaka 2017 na kuongeza kuwa hadi sasa watu milioni 1.4 wanaishi na UKIMWI ukilinganisha na mwaka 2012 ambapo palikuwa na watu milioni 1.6 walioishi na UKIMWI.
“Zaidi ya Watu 72,000 hupata maambuki mapya ya UKIMWI kila mwaka na watu 78,000 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na UKIMWI,” alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa