Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amwataka wamiliki wa maeneo ya starehe, nyumba za kuabudia na studio Mkoani Rukwa kuzingatia kanuni, sheria na miongozo ya udhibiti wa kelele.Ameeleza kelele zinazopita kiasi zina athari kubwa kwa jamii.
Mheshimiwa Makongoro ameyasema hayo leo Juni 27,2023 akiwa katika kikao na wamiliki wa studio, kumbi za sterehe na mikutano, maeneo ya kuabudia(viongozi wa dini) na wafanyabiashara mbalimbali kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na NEMC kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema pamoja na kuwa tatizo la kelele sio kubwa katika Mkoa wa Rukwa Serikali inabaki na dhamana na wajibu wa kuchukua hatua za udhibiti mapema.
Imeelezwa kuwa kelele zinazozidi viwango vilivyowekwa kikanuni zina athari kubwa kwa jamii, athari zinazotajwa ni pamoja na waathirika kukosa usingizi, mataizo ya usikivu, kuongezeka kwa mapigo ya moyo kusiko kwa kawaida na kupelekea shinikizo la damu na hata mimba kuharibika.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa amewataka washiriki kwa pamoja kuzuia uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na kelele kwa kuhakikisha kanuni miongozo na sheria za udhibiti wa kelele zinazingatiwa.
Ameshauri elimu kuendelea kutolewa na ikibidi kuwa na vipimo vya sauti ili kuhakikisha jamii inakuwa salama bila changamoto zinazosababishwa na kelele.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa