Rais wa Tanzania Mh. John Pombe Magufuli amesema uchaguzi umekwisha na kazi kubwa iliyo mbele yao ni kudumisha amani, utulivu, kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimataifa na kukamilisha miradi ya maendeleo.
Rais Magufuli ameitoa kauli hiyo mjini Dodoma, mara baada ya kula kiapo cha urais cha kulitumikia taifa hilo la Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka mitano kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli amesema kuwa amani na mshikamano vilivyopo nchini Tanzania vinapaswa kudumishwa na kwamba uchaguzi umekwisha na Watanzania wajikite zaidi katika kuchapa kazi hivi sasa kama ilivyo kauli yake tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka 2015.
Aidha, Rais Magufuli ameongeza kusema kuwa anaishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC kwa kuendesha na kusimamia uchaguzi huo uliomalizika kwa amani na utulivu Oktoba 28.
Katika sherehe hizo zilizofanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma tangu kuasisiwa kwa taifa la Tanzania, viongozi wa nchi 20 wakiwemo maraisi kutoka Uganda, Comoro, Zimbabwe pamoja mabalozi 83 wamehudhuria.
Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, akitoa salaam zake za pongezi kwa Rais Magufuli mara baada ya kuapishwa kwake, amesema kuwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hazina budi kuongeza mshikamano na kutanua masoko ya ndani ili ziweze kujitegemea na kuhakikisha uchumi wa nchi hizo unakuwa.
Aidha, Rais Museveni amesema kuwa tatizo la baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika wamegawanyika baada ya kupata uhuru.
Hata hivyo, katika kiapo hicho cha Rais Magufuli pia aliapishwa makamu wake Mh. Samia Suluhu Hassan.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa