Sumbawanga- Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, ametoa pongezi kwa watahiniwa wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita (ACSEE) Mwaka 2025 kufuatia kupanda kwa kiwango cha ufaulu Mkoani Rukwa.
Taarifa iliyotolewa Julai 07, 2025 na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) inaonesha kuwa Mkoa wa Rukwa ulikuwa na watahiniwa 2,034 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Sita 2025.
Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa watahiniwa wote 2,034 wamefaulu kwa viwango vya daraja la kwanza hadi la tatu huku kukiwa hakuna daraja na nne na daraja sifuri hali inayoashiria kupanda kwa viwango vya ufaulu Mkoani hapa.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Sita 2025 kutoka kwa Afisa Elimu wa Mkoa, Mheshimiwa Makongoro amesema kupanda kwa viwango vya ufaulu ni matokeo ya ushirikiano thabiti kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na Serikali.
Amewapongeza walimu, wazazi na watahiniwa kwa kazi nzuri na kuendelea kuiweka Rukwa katika ramani ya mafanikio kitaaluma.
Taarifa ya Baraza la Mitihani inaonesha kuwa watahiniwa 1,110 kati ya watahiniwa 2,034 wamepata daraja la kwanza la ufaulu sawa na asilimia 54.6, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.3 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 53.3 cha Mwaka 2024.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa