Waziri wa Elimu nchini Prof. Joyce Ndalichako amethibisha kuunda kamati itakayoshughulikia namna mkandarasi anayeendelea na ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Rukwa alivyopata zabuni na kumtaka mkandarasi huo ajieleze sababu zilizopelekea kuidanganya serikali katika mkataba wake ulioonyesha uwepo wa vifaa vya kazi katika eneo la ujenzi huku eneo hilo likiwa tupu na kazi zake kufanyika bila ya wataalamu na vifaa vilivyoorodheshwa kwenye mkataba.
Ameongeza kuwa Kamati hiyo pia itashughulikia kuona endapo thamani ya fedha iliyotolewa na serikali inaendana na majengo yaliyojengwa katika eneo hilo ambalo yalitakiwa kujengwa majengo 22 ambapo hadi sasa ni majengo 13 tu kikiwepo kibanda cha mlinzi ndio yameanza kuinuka. Wakati mkandarasi hiyo akitakiwa kukabidhi majengo hayo mwezi Septemba 2019 hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 25 tofauti na makubaliano ya mkataba aliotakiwa kufikia asilimia 61 hadi mwezi Mei.
Katika kuhakikisha wahusika wanashughulikiwa Prof Ndalichako alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na kumuidhinisha mkandarasi (post qualification) aliyepewa zabuni pamoja na kumtaka kumchukulia hatua Mkurugenzi wa VETA kanda ya nyanda za juu kusini kwa kuonyesha kumtetea mkandarasi ambaye hana uwezo wa kazi.
“Wakandarasi wanaofanya kazi na Wizara ya Elimu badilikeni, kwakweli miradi yangu yote nitaendelea kuipitia na nitaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wakandarasi ambao wanapata kazi kwa kiujanja ujanja, kwanza nitashughulika na watu wangu wa kitengo cha manunuzi, hebu angalia vifaa kama hivyo, kuna Afisa wa wizara ambae anapata mshahara ate serikali na alikwenda akathibitisha akasema vifaa viko vizuri akaandika na ripoti, naoma Mkurugenzi Mkuu anza na hao waliofanya “post qualification” kabla y ahata kamati haijaja kufanya kazi wengine ambao watakumbwa sasa ni baada ya kamati kufanya kazi, lakini Mkurugenzi wako wa Kanda hakufai kwasababu anaonekana yeye ni dalali wa Mkandarasi” Alisisitiza.
Amesema hayo baada ya kutembelea ujenzi wa chuo cha ufundi Stadi VETA katika eneo hilo la Kashai lililopo katika Manispaa ya Sumbawanga na kuonyesha kutoridhishwa na kuelekeza kuwa kabla ya kuendelea na ujenzi huo lazima vifaa vinavyotumika katika ujenzi vipimwe kuonyesha kama vinastahili ama vinginevyo viondolewe katika eneo la ujenzi na mkandarasi huyo kuleta vifaa vingine kwa gharama yake.
Awali wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho Mkurugenzi wa Kanda wa chuo cha VETA Justine Rutta alisema kuwa changamoto kubwa iliyokuwapo ni mkandarasi huyo kucheleweshewa malipo yake na hivyo anaidai serikali shilingi 51,039,153.59 hali iliyosababisha kuchelewa kuendelea na ujenzi.
“Kwahiyo kwenye hela nayotakiwa kulipwa inaongezeka deni hilo ambalo ni kwaajili ya kucheleweshewa ulipaji, hali ya malipo kwa mshauri wa mradi, ameshalipwa tayari shilingi 1,051,144,000 tangu aanze kufanya kazi hii na nyingine alitakiwa kulipwa mara atakapofikia hatua ya kuweka sakafu, kwahiyo hatudai fedha yoyote mpaka sasa, changamoto katika mradi huu ndio kubwa mradi umeweza kuchelewa kwasababu ya kuchelewa kulipwa kwa mkandarasi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alibaini uwepo wa kampuni nyingine mbili zinazohusika na ujenzi wa chuo hicho, kampuni ambazo serikali haikuingia nazo mkataba na baada yakuulizwa mhandisi wa ujenzi huo (site engineer) aliyefahanmika kwa jina la Jin alisema kuwa kampuni hizo zilisaini mkataba na Tender International kwaajili ya kuwapata vijana wa kufanya kazi, kuwasimamia pamoja na kusimamia malipo ya vijana hao.
Prof. Ndalichako alisikitishwa na kitendo cha mkandarasi huyo kuingia mikataba na kampuni nyingine ambazo hazikidhi viwango vya utekelezaji wa miradi ya serikali kwani kati ya kampuni hizo moja inayoitwa Aricom Building Constractors limited ilikuwa na daraja 7 na nyingine Laicom Building Construcors ilikuwa na daraja 4. Na aliyagundua hayo baada ya kutaka kuonyesha mikataba ya wafanyakazi wa ujenzi huo.
Tarehe 31/8/2019 mkandarasi Tender International alikabidhiwa kiwanja kwaajili ya kuanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Manispaa ya Sumbawanga ambapo mshauri Elekezi wa Mradi huo ni Sky Architect Consultancy Ltd na mradi huo kutegemewa kukamillika mwezi Septemba 2019 huku gharama za mradi huo ikiwa shilingi 10,700,488,940.05 na tarehe 22/11/2018 alilipwa shilingi 1,272,138,424.64. na tarehe 11/4/2019 alilipwa shilingi 835,598,299.01 na kufanya jumla ya Shilingi 2,107,736,723.65 ya malipo kwa Mkandarasi huyo ambayo ni sawa na asilimia 25 ya malipo yote.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa