Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Rukwa imekamilisha ahadi yake kwa wananchi ya kuwapunguzia changamoto ya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kukamilisha ujenzi wa Daraja la Mto Kalambo.
Mbali na daraja hilo, Barabara ya Sumbawanga Matai hadi Kasanga port (112km) Kilomita 71.4 zimeshawekwa lami.
Akizungumza mara baada ya kukagua daraja na barabara hiyo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi. Edwin Ngonyani, amesema kukamilika barabara hiyo kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa mkoa Rukwa na nchi nyingine za jirani ikiwemo Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi.
"Tuliwaahidi wananchi kujenga daraja na barabara hii ili wafanyabiashara na wakulima waweze kusafirisha bidhaa na mazao yao kwenda katika masoko kwa wakati na hivyo kukuza uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Mhandisi. Ngonyani.
Ameongeza kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali itahakikisha ndani ya kipindi cha miaka mitano inakamilisha ahadi zote walizoahidi kwa wananchi ili wananchi wanufaike na Serikali yao.
"Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ipo kwa ajili ya wananchi wote, na sisi kama wasimamizi tuliopewa dhamana kwenye wizara tutahakikisha kile tulichokiahidi kwa wananchi tunakitekeleza kwa wakati ili wananchi wanufaike na uchumi wa nchi ukue,” amesisitiza Waziri Ngonyani.
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Rukwa, Mhandisi. Msuka Mkina amewataka wananchi kutunza miundombinu ya barabara na kuacha vitendo vya kung'oa alama za barabarani ambazo zimewekwa ili kuongeza usalama kwa madereva katika matumizi ya barabara hizo.
"Tumeweka alama hizi barabarani kwa ajili ya kuongoza madereva wanaotumia barabara ili kuepusha ajali zinazoweza kutokea kwa kutokuwepo na alama za tahadhari, hivyo ni wajibu wenu kuzilinda na kuzitunza kwani zipo kwa faida yetu sote,” amesema Mkina
Katika hatua nyingine Waziri Ngonyani amekagua huduma za bandari ya Katanga na kusema Serikali itaendelea kuziboresha bandari zilizopo Ukanda wa Ziwa Tanganyika ili kuvutia wasafirishaji wa mizigo mikubwa kutumia bandari hizo.
"Tutaendelea kuimarisha miundombinu ya bandari za Kalema, Kigoma na Katanga ili ziwe na uwezo wa kupakia na kupakua mizigo mikubwa kwenda DRC na Burundi,” amesisitiza Ngonyani.
Naye Msimamizi wa Bandari Mkoa wa Kigoma, Morris Mchindiuza amesema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imejipanga na imetenga kwenye bajeti yake Sh. 1 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa gati namba moja na hivyo kuchochea ukuaji wa kibiashara na ongezeko la meli hususan nchi za jirani kama Burundi na DRC.
Naibu Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, ujenzi wa nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu, bandari na madaraja katika mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa