UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE SUMBAWANGA WAFIKIA ASILIMIA 80; RC MAKONGORO APONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI
Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere, amefanya ziara ya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga leo Julai 22, 2025 na kueleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji, ambapo kwa sasa ujenzi huo umefikia asilimia 80.
Katika taarifa ya maendeleo ya mradi huo, msimamizi wa ujenzi wa mradi huo Bw. Joseph Stephen Jimonge ameeleza kuwa tayari maeneo muhimu kama uwekaji wa tuta la kushukia ndege umekamilika kwa asimilia 100, eneo la maegesho ya magari kwa asilimia 98, mitaro ya maji kwa asilimia 98 na barabara ya kuingia uwanjani yamekamilika kwa asilimia 96. Ujenzi wa jengo la abiria kwa sasa umefikia hatua ya asilimia 85, huku mradi mzima ukitarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mheshimiwa Makongoro amesema kukamilika kwa kiwanja hicho kutakuwa chachu kubwa kwa uchumi wa Mkoa wa Rukwa kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, bidhaa, pamoja na kufungua fursa mpya za uwekezaji hasa katika sekta ya madini kama vile shaba, helium, na chuma.
“Kukamilika kwa kiwanja hiki ni hatua muhimu katika kuiunganisha Rukwa na mikoa mingine, na pia na nchi jirani. Ni fursa ya kiuchumi ambayo italeta mageuzi makubwa kwa wananchi wetu,” amesema RC Makongoro.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa