Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Charles Makongoro Nyerere, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhakikisha miradi inakamilishwa kwa wakati uliopangwa na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Makongoro ametoa maelekezo hayo leo Januari 28, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani humo iliyolenga kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji na miundombinu.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa Shule ya Msingi Katani, ujenzi wa Kituo cha Afya Kasu, shule ya msingi ya mkondo mmoja Milundikwa pamoja na maendeleo ya ujenzi wa shule ya amali. Aidha, amekagua na kuzindua mradi wa maji eneo la Majengo, Chala.

Akizungumza na viongozi wa Wilaya, watendaji wa Halmashauri na wakandarasi, Mheshimiwa Makongoro amesisitiza kuwa ucheleweshaji wa miradi unawanyima wananchi haki ya kupata huduma bora, na kuwataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji.
Vilevile, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi hiyo na kuitunza ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu, akibainisha kuwa miradi hiyo ni mali ya wananchi wenyewe.
Ziara hiyo imehitimishwa kwa kikao cha tathmini kilichofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya, ambapo Mkuu wa Mkoa amepokea taarifa za utekelezaji wa miradi na kutoa maelekezo ya kuboresha maeneo yaliyobainika kuwa na changamoto.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa