Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani amesema zoezi linaloendelea la kusambaza umeme vijijini kupitia mradi wa REA litapunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini na kubaki vijijini kwakuwa mradi huo una lengo la kusogeza fursa za kiuchumi zinazotegemea umeme katika maeneo yao.
Amesema kuwa serikali inatambua kuwa kuna uhitaji wa umeme mkubwa ingawa umeme unaozalishwa kwa sasa unakidhi mahitaji yaliyopo katika mkoa wa Rukwa ila mahitaji yanategemewa kuongezeka kadiri uchumi wa viwanda utakavyozidi kukuwa hivyo ni jukumu la serikali kujiandaa kukabiliana na hali hiyo.
“Hii nyanda ya Kaskazini magharibi kuanzia Mbeya, Sumbawanga, Mpanda hadi Kigoma kuna shida ya umeme mkubwa ingawa sasa umeme upo lakini ni wa gharama kwasababu ni wa mafuta na ni mkakati wa serikali kuleta umeme mkubwa, tulishaanza hatua za awali za ujenzi wa umeme mkubwa wa KV 400 kutoka Mbeya – Sumbawanga – Mpanda hadi Kigoma mrdi unaotegemewa kumalizika July 2019,” Amesema.
Awali akisoma taarifa ya hali ya umeme katika Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachima Wangabo amebainisha uwepo wa viwanda 26 vinavyohitaji huduma ya umeme ikiwemo viwanda vya kusindika nafaka na Samaki.
“Tumefanya tathmini na kubaini viwanda 26 ombi letu kwako ni kutusaidia viwanda hivi viweze kupata umeme kwa sababu uendeshaji wake ni ghali sana kwa sasa. Baadhi ya viwanda hivyo vimefungwa kwa sababu havina nishati hiyo ya Umeme.”Mh. Wangabo alibainisha.
Mkoa wa Rukwa unapata umeme kutoka nchi jirani ya Zambia. Pamoja na kupata umeme kutoka kwenye gridi ya Zambia Mkoa wa Rukwa una mashine nne zinazotumia mafuta mazito (IDO). Umeme unaozalishwa kupitia mifumo hiyo ni Megawati 9.5 ikiwa 5MW ni za mashine na 4.5MW za gridi ya Zambia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa