Jamii imeaswa kuimarisha upendo na maadili ili kupata familia imara. Uimara wa familia utajenga jamii imara na kupunguza ukatili wa kijinsia, utoro mashuleni, lishe duni na mimba za utotoni.
Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Mei 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Queen Cuthbert Sendiga katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya familia duniani.
Mheshimiwa Sendiga amesema ikiwa kila mwanafamilia atatimiza wajibu wake kikamilifu na kutoa kipaumbele kwa upendano wa ndugu, maadili na malezi bora kuna uwezekano mkubwa wa kukomesha matendo ya kikatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii. Amesema masuala hayo yanaweza kupunguza pia kusambaratika kwa familia.
Ameishauri jamii ya Rukwa kutengeneza utaratibu wa kukaa pamoja na kushauriana katika mambo mbalimbali, kukosoana kwa hekima pindi mmoja wa wanafamilia anapokengeuka na kupongezana kwa mazuri yanayofanyika ndani ya familia, akieleza kuwa kwa kufanya hivyo familia zitaimarika, upendo utaongezeka, maadili yataimarika na familia zitadumu.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa