Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia chakula unaoendelea kujengwa katika eneo maalum lililotengwa na Manispaa ya Sumbawanga kwaajili ya uwekezaji wa viwanda pamoja na maghala lililopo Kanondo katika Kata ya Ntendo na hivyo kuwataka wamiliki wengine walionunua viwanja katika eneo hilo kuhakikisha wanawekeza ili kuongeza ajira.
Amesema kuwa ujenzi huo wa vihenge ni mkubwa na unagemewa kutoa ajira mbalimbali na hivyo kuwataka wananchi wa mji wa sumbawanga na maeneo mengi ya Mkoa kutoa kuchangamkia fursa ya ajira katika ujenzi utakaogharimu karibu shilingi bilioni 15 na hivyo kuwataka Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) Sumbawanga kuhakikisha wanasimamia vizuri kwa msaada na ushauri kutoka Wakala wa Majengo Tanzania wakihakikisha mkandarasi hafanyi makosa.
“Tulichelewa kuanza huu ujenzi lakini tulitaka huu ujenzi wa vihenge uje katika eneo hili la viwanda la Kanondo, Hii kazi naona mmeanza vizuri pamoja na kuchelewa tangu mwezi wa saba, tunategemea mwezi wa saba mwakani hivi vihenge sita viwe vimekamilika pamoja na ghala lake moja na uwezo wa vihenge pamoja na ghala ni kuhifadhi tani 26,000 na vikikamilika NFRA watakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 59,500 hii ni mara mbili ya uwezo tulionao sasa hivi, hivyo tunawahamasisha wakulima walime mahindi kwa wingi, uhakika wa soko upo,” Alisisitiza.
Wakati akitoa taarifa ya ujenzi huo Meneja wa NFRA kanda ya Sumbwanga Abdillah Nyangasa alisema kuwa NFRA wana maghala katika maeneo matatu ndani ya mkoa wa Rukwa moja likiwa Halmasharu ya Wilaya ya Sumbawanga katika mji mdogo wa Laela na mawili yakiwa katika Manispaa ya Sumbawanga katika eneo la Mazwi pamoja na eneo la Kanondo.
“Kwa upande wa Mazwi tuna maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 18,500 ambapo hali yake mengi ni machakavu yanahitaji ukarabati pia mazwi hapo hapo tuna ghala la tani 4000 ambalo nalo ni chakavu na lilitakiwa kufanyiwa ukarabati kama mradi huu ungefanyika pale lakini hapo mazwi kuna maghala mawili ya tani 3000 na kufanya tani 6000 ambayo hayo hayahitaji ukarabati na ndipotulimohifadhia mahindi, lakini kuna ghala la Laela ambalo lina uwezo wa kuhafadhi tani 5000 hili linahitaji ukarabati kidogo kwa ndani, lakini pia kuna mradi huu mpya wa kanondo,” Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema kuwa Eneo hilo la Viwanda na maghala lina viwanja 103 na viwanja 43 tayari vimeshauzwa na kuongeza kuwa ujio wa ujenzi wa vihenge hivyo utasaidia kuongeza thamani ya eneo hilo kwasababu ilikuwa inaonekana miundombinu bado haijafika lakini kutokana na ujenzi wa vihenge hivyo halmashauri imefanikisha kufikisha umeme na maji katika eneo hilo na kuongeza kuwa Manispaa inamradi mkubwa wa maji unaotarajiwa kusambaza maji katika eneo hilo.
“Tunawaomba wananchi wa Sumbawanga na wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza kwani sasa eneo letu lipo hai na limeanza kufanyiwa kazi, waje wawekeze viwanda mbalimbali, hata wafanyabiashara wetu wa pale mjini lakini mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa kuongeza tunategemea nasi Manispaa kuchukua viwanja viwili ambapo tutajenga sehemu kwaajili ya wafanyabiashara wadogowadogo walipo pale mjini waweze kuhamia hapa,” Alimalizia.
Ujenzi huo wa vihenge vipya vya kisasa unaojengwa na mkandarasi Elerai Construction Company Limited kwa ufadhili wa Serikali ya Poland wenye thamani ya Shilingi bilioni 13.6 unatarajiwa kumalizika mwezi July, 2020 na kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kutoka tani 33,500 za sasa hadi kufikia tani 59,500 na hivyo kuongeza ununuzi wa zao la mahindi wa NFRA kutoka kwa wakulima.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa