Wanachama na viongozi wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TADEDEA) kwa kushirkiana na Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Mkoani Rukwa wameridhishwa na elimu ya kutambua aina mbalimbali za kemikali zinazoweza kuwaathiri wakati wakijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii.
Akiongea mara baada ya Semina fupia iliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya Mbeya Mwenyekiti wa CHAVITA Mkoani Rukwa Henry Kisusi alisema kuwa pamoja na kufurahishwa na uelewa walioupata kutokana na mafunzo hayo ni vyema mamlaka hiyo na taasisi nyingine zinazolenga kutoa mafunzo kwa viziwi zikaona namna ya kutumia lugha ya Kiswahili katika mawasilisho yao na vipeperushi kuliko kutumia kiingereza mabcho wengi hawakifahamu.
“Tunaomba wabadili changamoto za mada mbalimbali zinazotolewa, kuna mada nyingine zinatolewa kwa lugha ya kiingereza, wakati viziwi wengi ufahamu wa lugha ya kiingereza hawana na wapo ambao hawajui lugha ya alama, hivyo wanatumia macho katika kusoma kile mabacho kinaonyeshwa ubaoni, hivyo lugha hiyo inakwamisha uelewa wa mada nzima ya athari za serikali,” Alisema.
Aidha kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TADEDEA Kelvin Mnyema aliiomba serikali ya Mkoa wa Rukwa kuona namna ya kuwasaidia Viziwi ambao wanajishughulisha na na Kilimo kwani wamekuwa wakipata changamoto kubwa katika kusafirisha mazao pamoja na kupata masoko.
Katika kulijibia hilo Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa David Kilonzo alithibitisha kuwa serikali ya Mkoa itahakikisha inatatua tatizo hilo pamoja na kero zilizowasilishwa na Chama hicho cha Viziwi na kuongeza kuwa Katiba ya Tanzania inampa haki kila mmoja bila ya kujali ulemavu walionao.
“Tumepokea orodha ya wakulima ambao wakati mwingine wakipata shida wakati wakisafirisha mazao yao kwenda sokoni, tumeyapokea, na kama serikali ya Mkoa tunaahidi kwamba tutawasaidia kumaliza kero kila tutakapokuwa tunazipokea, kama mnavyofahamu kwa mujibu wa katiba ya nchi yet una Ilani ya CCM ambayo ndiyo inayoongoza serikali imeweka pia katika vipaumbele vyake, masuala muhimu kwaajili ya watu wenye ulemavu,” Alisema.
Kwa upande wake Mkaguzi wa Kemikali kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kanda ya Mbeya Rashid Mjema alisema kuwa elimu ya Kemikali ni kwaajili ya watu wote hata wale wasiojishughulisha nazo kwasababu ni vitu ambavyo vinatuzunguka kuanzia mashambani hadi barabarani.
“Tukienda maeneo mbalimbali kwa mfano migodini kuna Kemikali, mashuleni kuna kemikali, kwahiyo hili kundi tuliona ni muhimu na wao wakapata hii fursa kwasababu ni haki yao ya msingi kwa lengo la kulinda afya pamoja na mazingira, kwahiyo hatutaishia kwao tu pia tunafundisha wajasiliamali wanaotengeneza batiki, sabuni, vipodozi na vitu kama hivyo,” Alimalizia.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa