Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakurugenzi kutosheherekea sikukuu ya Christmas mpaka watakapopata ufumbuzi wa ujenzi wa madarasa 99 yanayohitajika kwaajili ya kutumiwa na wanafunzi 4930 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka 2019.
Amesema kuwa ufaulu mwaka huu 2018 umekuwa kwa asilimia 73 ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo ulikuwa ni wa asilimia 68 na hivyo wanafunzi 4930 kukosa kuingia madarasani kutokana na changamoto ya upungufu wa madarasa.
Ameongeza kuwa serikali ya Mkoa imejipanga vilivyo kuhakikisha hakuna hata mwanafunzi mmoja anakosa nafasi ya kusoma hali ambayo itawafanya wanafunzi wote waliokosa nafasi kupatiwa fursa ya kuendelea na masomo yao kwa mwaka 2019 na kuwaomba wanachi kwa kushirikiana na halmashauri kuhakikisha vyumba hivyo vinapatikana hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa pili.
“Hawa wanafunzi tusiwakatishe tamaa ya kukosa nafasi ya kwenda kidato cha kwanza, hakuna mwanafunzi hata mmoja ataacha kwenda kidato cha kwanza, wakuu wa wilaya wote wasimamie zoezi hili na hakuna likizo na wale wakurugenzi wote hakuna kwenda likizo mpaka vyumba vya madarasa vyote view vimekamilika,” Alisema.
Ametoa maagizo hayo wakati akitoa salamu zake za Christmas kwa wananchi wa mkoa wa Rukwa na kuwatakia wananchi wote kusherehekea sikukuu hiyo pamoja na kuukaribisha mwaka mpya kwa amani na utulivu kwani walianza vizuri na wamalize vizuri na kuwaomba kuendeleza mshikamano na ushirikiano kwa miaka inayofuata.
Kati ya hayo madara 99, halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga inatakiwa kujenga madarasa 41 yatakayotumiwa na wanafunzi 2,042, huku Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikihitaji madara 27 ili kutumiwa na wanafunzi 1,365 na halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ikihitajika kujenga madarasa 19 kwaajili ya wanafunzi 925 na halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ikitakiwa kujenga madarasa 12 kwaajili ya wananfunzi 598.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa