Na Khadija Dalasia - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa
Tarehe: Septemba 15, 2023
Waganga Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Songwe, Katavi, Mbeya na Kagera wametakiwa kukamilisha maandalizi ya kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya Polio inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba 2023.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ametoa maelekezo hayo leo tarehe 15 Septemba 2023 alipofanya kikao na watumishi wa sekta ya Afya Mkoani Rukwa.
Profesa Nagu ametoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya zilizomo katika Mikoa hiyo kukamilisha maandalizi kabla ya tarehe hizo.
Amesema kuwa Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababisha ulemavu wa viungo na unaoweza kusababisha kifo. Njia mojawapo ya maambukizi ni kupitia kinyesi hivyo ametaka wananchi wote wakumbushwe na kuelekezwa kuwa na vyoo bora na kuvitumia kwa usahihi.
Amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa miaka nane kushuka chini anafikiwa pasipo kujali changamoto za kijiografia.
Amewaelekeza kuhakikisha chanjo inapatikana katika maeneo yote yaliyotengwa kwa shughuli hiyo na kuhakikisha hamasa kwa wananchi inatolewa kupitia viongozi wa kidini, watu mashuhuri kijamii na kwa kupitia vyombo vya habari na kurasa za mitandao ya kijamii.
Mkakati maalum umewekwa ili kuhakikisha chanjo hiyo inawafikia watoto wanaoishi katika maeneo ya mbali na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa kuwa na timu zitakazotoa huduma tembezi.
Profesa Tumaini Nagu ameyashukuru mashirika ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF, kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kutokomeza Polio.
Watoto 391,883 wanatarajiwa kuchanjwa katika Mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa