Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Cuthbert Sendiga amewaasa waandishi wa Habari Mkoani Rukwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia misingi na maadili ya uandishi wa habari.
Ameyasema hayo tarehe 13 mei 2023 katika siku ambayo umoja wa waandishi wa Habari Mkoani Rukwa wameadhimisha siku ya uhuru wa vyombo habari duniani kimkoa. Kauli mbiu ya Mwaka huu ni “Kuunda mustakabali wa haki kama kichocheo cha haki nyingine zote za binadamu”.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mkuu huyo wa Mkoa aliyekuwa mgeni rasmi katika tukio hilo amewapongeza waandishi wa habari wa Mkoa wa Rukwa kwa kazi nzuri ya kuutangaza Mkoa na fursa za kiuchumi zilizopo. Pamoja na pongezi hizo mkuu wa mkoa amewaasa waandishi wa habari kuisaidia jamii ya Rukwa kwa kuielemisha huku wakizingatia misingi na maadili ya habari. Ameeleza kuwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa bado wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo changamoto za lishe duni, ukatili wa kijinsia na uharibifu wa mazingira. Amewaomba wanahabari kutumia kalamu na sauti zao kukabiliana na changamoto hizo huku akiwasihi kuieleza jamii hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto zao lakini pia kuhamasisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi katika kukabiliana na changamoto zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia kwa kuendeleza juhudi za kuimarisha uhuru wa habari. Amewaelekeza Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Rukwa kuweka utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari ili waweze kupokea Habari ziznzowahusu wananchi wao na kutoa Habari kuhusu namna Serikali inavyokabiliana na changamoto hizo. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema mwandishi wa habari ni jicho na sikio na ni msaada kwa ufanisi wa Serikali.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa