RUKWA KUFANYA MAPINDUZI YA ELIMU
Na.OMM Rukwa
Wadau wa elimu mkoa wa Rukwa wameazimia kuongeza jitihada katika kukuza sekta hiyo ili kuondokana na kushuka kwa ufaulu miongoni mwa wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Rashid Mchatta wakati akiwasilisha salamu za mkoa kwenye mkutano wa sekta ya elimu ulioandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI mjini Sumbawanga (Jumamosi 14 Januari,2023) .
Mchatta alisema mkoa huo umeweka mikakati ya kuinua kiwango cha ufaulu ikiwemo kuhakikisha shule zote zinakuwa na walimu, vifaa vya kufundishia na miundombinu mizuri na ya kutosheleza kufuatia serikali kutoa shilingi Bilioni 3.7 za elimu bila ada kati ya Julai na Desemba 2022.
“Ufaulu wa mkoa umeshuka toka asilimia 80.15 mwaka 2021 hadi asilimia 77.9 mwaka 2022 kwa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, mtihani wa darasa la nne mkoa umeshuka toka asilimia 79.95 mwaka 2021 hadi asilimia 75.6 mwaka 2022, mtihani wa kidato cha pili umeshuka toka asilimia 92 mwaka 2021 hadi asilimia 63.3 mwaka 2022” alisema Mchatta.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Elimu TAMISEMI Vicent Kayombo alisema taarifa zinaonyesha bado kuna wanafunzi wanamaliza darasa la saba bila kuwa na umahili na kuwa serikali imepanga kuondoa tatizo hilo.
Kayombo alibainisha mikakati itakayosaidia kukuza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kuwa ni kuhakikisha utoro wa wanafunzi unadhibitiwa pamoja na shule kuendelea kutoa chakula cha mchana .
Mkutano huo uliwakutanisha walimu wakuu, wakuu wa shule na maafisa elimu kata toka halmashauri zote nne za Sumbawanga, Nkasi, Kalambo na Manispaa ya Sumbawanga na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga kwa niaba ya Waziri wa Nchi Tamisemi Angela Kairuki.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa