Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (iNEC), Bw. Martin Mnyenyelwa, ametoa wito kwa wadau wa uchaguzi Mkoani Rukwa kuwa mabalozi wa uhamasishaji kwa wananchi ili wajitokeze kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura kuanzia tarehe 12- 18 Januari 2025.
Mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura umefanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga leo tarehe 31 Desemba 2024.
Akizungumza Katika Mkutano huo Ndg.Martin Mnyenyelwa amesema kuwa lengo la mkutano huu ni kuwapatia wadau taarifa muhimu kuhusu zoezi hili la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura . Bw. Mnyenyelwa aliwasihi viongozi wa vyama vya siasa na wadau wote kuheshimu sheria, kanuni, na maelekezo ya iNEC na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuathiri mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura vituoni.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wadau kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa asasi za kiraia, waandishi wa habari, wawakilishi wa makundi ya vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, na Wazee wa Kimila.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa