WAFANYABIASHARA RUKWA LIPENI KODI KWA WAKATI-
RC MKIRIKITI
Wafanyabiashara wa mkoa wa Rukwa wametakiwa kuwa na mtindo wa kulipa kodi kwa hiari ili kuwezesha serikali kupata mapato ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti jana (13.09.2021) wakati alipofungua semina ya utoaji elimu ya kodi iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mjini Sumbawanga.
“Ni vizuri wafanyabiashara wote mkawa na utaratibu wa kulipa kodi kwa hiari badala ya kusubiri mivutano kwani serikali inategemea fedha hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa umma” alisema Mkirikiti.
Katika semina hiyo iliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali wa mjini Sumbawanga, Mkirikiti aliwataka watumie pia fursa ya fedha zinazotolewa na serikali kwa miradi ya afya, shule na miundombinu ili washiriki ujenzi wa miradi hiyo.
Mkirikiti aliongeza kusema serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuleta fedha nyingi za miradi ikiwamo Shilingi Milioni 750 za hii karibuni zilizotokana na tozo ya miamala ambazo zinakwenda kujenga vituo vitatu vya afya kwenye tarafa za mkoa wa Rukwa.
Mkuu huyo wa Mkoa alitaja vituo vya afya vitakavyojengwa kuwa ni Mwazye ( Kalambo), Kate ( Nkasi) na Kipeta ( Sumbawanga) ambapo kila kimoja kimepatiwa Shilingi Milioni 250 kwa awamu ya kwanza mwezi Agosti mwaka huu.
“Ninapenda wafanyabiashara wa Rukwa muwe na taarifa za miradi na fedha zinazotolewa na serikali ili iwe chachu kwenu kujitokeza kutekeleza na kutoa huduma ili mpate fedha pia serikali ipate kodi badala ya kuachia miradi hiyo wafanyabiashara toka nje ya Rukwa” alisisitiza Mkirikiti.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania Richard Kayombo alisema wapo mkoani Rukwa kuelimisha walipa kodi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari na kusikiliza changamoto zao.
Kayombo aliongeza kusema TRA itaendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato bila mikwaruzano ambapo msingi mkubwa ni kutekeleza Agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuona kodi inakusanywa kwenye mazingira rafiki sio kutumia nguvu.
Naye Anusisye Thomas mkandarasi wa ujenzi alitoa ombi kwa serikali ya mkoa kuwezesha wazabuni na wakandarasi wa ndani kupata kazi za miradi ya serikali ili wanufaike kiuchumi na kuwa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya mkoa wa Rukwa badala ya kutumia wakandarasi wa nje.
Mwisho
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa