Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere amewataka wananchi wa Kata za Kirando, Kipili na Kitete Wilayani Nkasi kutumia fursa ya mradi wa umwagiliaji unaojengwa katika Kata hizo kuinua kipato chao.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo Julai 23, 2024 aliposhuhudia utiaji saini na makabidhiano ya mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Lwafi - Katongolo kati ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Mkandarasi M/S Halem Construction Company Limited. Zoezi la makabidhiano ya mradi huo wenye thamani ya shilingi Bilioni 20.9 utakaotekelezwa kuanzia Julai 2024 hadi Julai 2026 limefanyika katika Kijiji cha Katongolo wilayani humo.
Mheshimiwa Makongoro amewaeleza wananchi kuwa lengo la Serikali ni kuwawezesha wakulima kufanya shughuli za kilimo muda wote wa mwaka pasipo kutegemea msimu wa mvua pekee.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Kata hizo kulinda miundombinu ya mradi ili uwe na manufaa kwa jamii kama ilivyokusudiwa na Serikali huku akimtaka Mkandarasi kuhakikisha anajenga na kutekeleza mradi kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa