WANANCHI WALIOVAMIA ZIWA RUKWA WAONDOSHWE- RC MKIRIKITI
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ametoa muda wa siku Thelathini kwa wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na makazi ndani ya eneo la mita Sitini kando ya Ziwa Rukwa kuondoka kwa kuwa wanasababisha uharibifu ikiwemo kupungua kwa kina cha ziwa hilo.
Mkirikiti alitoa kauli hilo juzi (08 Aprili 2022) mjini Sumbawanga wakati wa kikao cha wadau wa mazingira kilicholenga kuweka mikakati ya kunusuru uharibifu wa misitu na vyanzo vya maji kote mkoani.
Alisema ni wakati sasa kwa viongozi wa wilaya ya Sumbawanga wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Sebastian Waryuba kwenda na kuanza kutoa elimu kwa wananchi kupisha maeneo waliyovamia kwenye ukanda wa ziwa Rukwa kwa mujibu wa Sheria.
“Tuhakikishe eneo la mita Sitini kando ya Ziwa Rukwa likiwa bila watu wanaoishi au kufanya shughuli za kilimo na mifugo. Wote waliovamia waondolewe ndani ya siku 30 na nipatiwe taarifa ya utekelezaji .Viongozi nendeni mkasimamie sheria bila kuonea wananchi, “alisisitiza Mkirikiti.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Bonde la Ziwa Rukwa ilisema ziwa hilo lina ukubwa wa mita 88,000 ambapo lina kina cha mita tisa (9) ambazo zinaendelea kushuka kwa kasi kutokana na shughuli za binadamu hivyo tope jingi kujaa.
“Kwa upande wa Ziwa Rukwa kumekuwa na uharibifu mkubwa wa misitu ya Lyamba lya Mfipa hali inayosababisha ziwa Rukwa wakati mwingine kujaa tope. Hivyo wadau wa mazingira mnayo nafasi ya kuhakikisha kuwa mnawaelimisha wananchi kuutunza vyanzo hivi vya maji kwani maji ni uhai” Mkirikiti akihitimisha hotuba yake.
Akizungumza kuhusu uharibifu katika bonde la Ziwa Rukwa, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Sebastian Waryuba alisema ni kweli Mifugo, kilimo kando ya ziwa hilo pamoja na makazi yanaathiri uhai wa ziwa hilo.
Waryuba aliongeza kusema atatekeleza kazi ya kutoa elimu kwa wananchi wote waliovamia eneo hilo kwa kuwapa elimu juu ya sheria inavyotaka watu wakae umbali wa mita 60 toka ziwani na kuwa kazi hii itafanyika kwa weledi mkubwa.
Kilian Swai ni Afisa Utekelezaji toka Timu ya Mwanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) alisema uharibifu mkubwa wa mazingira unaendelea katika Misitu vya Lyamba lya Mfipa ambako ndio chanzo cha ziwa Rukwa usipodhibitiwa ziwa hilo litatoweka ndani ya miaka 50 ijayo.
Swai aliongeza kusema taasisi yake inafanya kazi na wananchi wa maeneo ya msitu wa Lyamba lya Mfipa kwa kugawa miche ya miti ya matunda na uhifadhi pamoja na kuisaidia kuwekwa kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili wananchi wasiendelee kuharibu mazingira .
Swai alisema taasisi hiyo imefanikiwa kusambaza miche ya miti 195,000 kati ya lengo la miche 300,000 ili kuhifadhi eneo la msitu wa Lyamba lya Mfipa ili wananchi watunze mazingira.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa ,Kamishna Msaidizi wa Polisi Theopista Mallya alishauri wataalam wa mazingira kutoa elimu kwa wananchi ili watambue kuwa kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji na Misitu ni kuvunja sheria kunakosababisha uwepo wa makossa ya jinai.
Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya namba 14 ya mwaka 2002 inakataza uharibifu wa Misitu unaotokana na ukataji holela wa miti kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa