Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuhakikisha anawapatia wanakamati ya upanuzi wa ujenzi wa kituo cha afya Kirando cheti cha uzalendo pamoja na kifuta jasho baada ya wanakamati hao kuonesha uvumilivu na kushirikiana na serikali katika upanuzi wa kituo hicho bila ya kudai posho ya aina yeyote.
Amesema kuwa pamoja na wanakamati wengine kukimbia kutokana na kukosa malipo ya aina yeyote wakati wakiendelea na usimamizi wa upanuzi wa kituo hicho cha Afya wao waliendelea kusimama imara ili kuhakikisha wanafanikisha zoezi hilo na hatimae wananchi wa Kijiji, Kata na Tarafa ya Kirando waweze kufaidika na juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya afya katika Mkoa wa Rukwa.
“Na mtayarishe Mkurugenzi cheti cha Uvumilivu, na mkono mtupu haurambwi mtayarishe na hata senti Fulani mle ndani iwe posho yao kwasababu hawajapata posho hata sumuni, kwahiyo muangalie mtajibana wapi ili cheti kiambatane na kifuta jasho tutakuwa tumewatendea haki na wengine wataiga,”Alisema.
Wakati akielezea siri ya kusimama imara Mwenyekiti wa kamati kituo cha afya Kirando ambae alikuwa mjumbe katika kamati ya ujenzi kwaajili ya upanuzi wa kituo hicho Seetbert Kapalata alisema kuwa anamshukuru mheshimiwa Rais kwa kuwafikiria watu wa Kijiji cha kirando na kuwapelekea mradi huo.
“Kweli tunamsukuru mheshimiwa Rais kwani ni jambo la kipekee sana ilikuwa sio rahisi kufikiria kwamba tunaweza kuapata kitu kama hiki miaka imepita mingi lakini hatujapata jambo kama hili kwahiyo ilikuwa ni lazi sisi tuunge mkono jitihada hizo, inawezekana akaja mwingine asifikieriea vituo vya afya akafikiria mambo mengine lakini bila ya afya hakuna kingine katika maisha,” Alisema.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa Kituo hicho ambae nae alikuwa katibu wa Kamati Dkt. Hashim Mvogogo wakati akitoa taarifa ya Kituo hicho cha afya alisema kuwa upanuzi huo umesaidia kuboresha huduma za upasuaji na maabara, jengo la wodi ya wajawazito pamoja na nyumba ya daktarin.
“Wodi ya akinamama imeboreshwa na hadi sasa jengo hilo lina uwezo wa kulaza kina mama 25 kwa wakati mmoja, vilevile chumba cha kujifungulia kina uwezo wa kubeba wajawazito wanne kwa wakati mmoja, hivyo tunaishukuru serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna alivyoweza kutuboreshea huduma katika kituo chetu,” Alimaliza.
Ujenzi wa Upanuzi wa Kituo cha Afya cha Kirando ulianza mwezi Februari mwaka 2018 na kumalizika mwezo Oktoba mwaka 2018 na kugharimu shilingi milioni 412 kwaajili ya ujenzi wa jengo la maabara, wodi ya wajawazito, jengo la upasuaji na nyumba ya daktari.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa