Wananchi Mkoani Rukwa wameunga mkono kusudio la Serikali la kulipumzisha Ziwa Tanganyika kwa muda maalum.
Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Kalambo katika kikao cha kutoa elimu kwa Madiwani, Watendaji wa Kata na viongozi wa vyama kilichofanyika leo Aprili 2, 2024, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo wameeleza kuwa kusudio hilo limepokelewa vyema na wananchi.
Wamesema kuwa wananchi wameanza kuchukua hatua mbadala za kupata samaki kwa kuwakausha ili kuwatunza kwa matumizi ya kipindi chote ambacho ziwa litakuwa limepumzishwa.
Pamoja na njia hiyo wananchi wamejiandaa kuendelea na shughuli za uvuvi katika mito, mabwawa ya kufugia samaki na maziwa mengine yaliyopo Mkoani Rukwa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mheshimiwa Lazaro Komba akizungumza katika kikao hicho ameipongeza Serikali kwa uamuzi huo na kuwataka viongozi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za kulipumzisha Ziwa, huku akiwataka kuwapa elimu endelevu ya ufugaji wa samaki na ulinzi wa wakati wote wa Ziwa hilo.
Serikali inatarajia kulipumzisha Ziwa Tanganyika kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia tarehe 15 Mei 2024 hadi tarehe 15 Agosti 2024 ili kutoa muda kwa samaki wa Ziwa Tanganyika kuzaliana na kukua kufikia kiwango kinachokubalika na kuruhusiwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa