Wananchi wa bonde la ziwa Rukwa wamepongeza serikali ya Mkoa wa Rukwa kwa juhudi za kuhakikisha mazalia ya samaki katika ziwa Rukwa yanaendelea kuwa salama kwa kupambana na wavuvi haramu wanaoharibu mazingira ya ziwa hilo.
Pongezi hilo zilijitokeza wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama iliyokwenda kuangalia usalama wa ziwa hilo na kufanikiwa kukamata nyavu haramu 188 zenye thamani ya wastani wa shilingi milioni 78 na kuzichoma mbele ya wananchi wanaoishi kwenye kambi ya wavuvi katika kijiji cha Ilanga, Kata ya Mfinga ili kuonesha mfano kwa wale wanaoendelea kutumia nyavu hizo kuharibu mazingira.
Zoezi hilo la kuchoma moto nyavu hizo haramu liliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Tixon Nzunda, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Halfan Haule pamoja na kamati za ulinzi na usalama ya Mkoa na Wilaya.
Katika kuhakikisha kuwa ziwa hilo linaendelea kutunzwa na kulindwa Mh. Zelote aliomba ushirikiano wa wananchi kuhakikisha wavuvi haramu wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua zinazostahiki ili iwe fundisho kwa wale wanaoendelea kufanya shughuli hizo bila ya kufuata taratibu na sheria.
“Hili ziwa ni lenu, Mkuu wa Mkoa wala Katibu Tawala hawaji kuvua samaki hapa, ni nyinyi, hivyo ni vizuri mkawa walinzi wa kwanza kabla serikali haijatumia nguvu nyingi kulinda eneo hili, Kila mmoja awe Mlinzi wa mwenzake na kila atakayetoa taarifa tutamlinda kwa sheria zilizopo,” Mkuu wa Mkoa alieleza.
Katika kusisitiza ulinzi huo Mh. Zelote alitoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kurudisha asilimia 20 ya mapato yanayopatikana kutokana na uvuvi ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi Paulo Mwang’onda alijitokeza kuipongeza serikali ya Mkoa wa Rukwa kwa juhudi zake za kuhakikisha wavuvi haramu wanakosa nafasi ya kuendelea kumaliza mazalia ya samaki.
“Naiunga mkono Serikali kuutokomeza uvuvi haramu, kwasababu wanaharibu mazalia ya samaki ambao ni faida kwa vizazi vyetu vijavyo, na naiomba serikali itupe ushirikiano pale tunapotoa taarifa za uvuvi haramu,” Paulo alisema.
Sambamba na hilo Mh. Zelote hakusita kuwakumbusha wananchi kuwa makini na ugonjwa hatari wa Ebola mbao upo katika nchi ya jirani y aJamhuri ya Watu wa Kongo (DRC) na kueleza kuwa ugonjwa huo hauna tiba na kuwaeleza dalili za ugonjwa huo.
“Dalili ni homa kali, kutapika, kulegea, kutokwa damu ndani na nje ya mwili na ikitokea umeumwa kimbilia zahanati, kwa daktari, usiseme nanunua Panadol, serikali ya Tanzania haitaki kuwapoteza watu wake.” Mh. Zelote Alifafanua.
Na katik kuhakikisha wananchi hao wanaondokana na udumavu, Mh. Zelote aliwasisitiza wananchi hao kuwa na utaratibu wa kuhifadhi chakula cha kutosha na kuacha kuuza mazao yote wanayovuna kwa lengo la kupata pesa huku wakiwa hawana chakula.
Katika kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa katika bonde la ziwa Rukwa Mkuu wa Mkoa aliahidi kutoa mifuko ya “Cement” 150 ili kumalizia ujenzi wa vituo viwili vya polisi, mifuko 100 kwa kituo cha polisi cha Mtowisa na mifuko 50 kwa kituo cha polisi cha Ilemba.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa