Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanafanya msako kwa wale wote waliohusika kuharibu na kung’oa ‘reflectors’ zilizowekwa kwenye vyuma vya kingo za barabara katika darala la Momba lililopo mpakani mwa Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe katika Bonde la Ziwa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga.
Amesema kuwa ung’oaji huo wa ‘reflectors’ hizo unaweza kusababisha ajali itakayopelekea kupoteza maisha ya watu nyakati za usiku na kupoteza malengo ya ujenzi wa daraja hilo na kuonya kutoendelea kwa uharibifu huo wenye lengo la kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi, mkoa na nchi kwa ujumla.
“Jeshi la Polisi mzisake bodaboda zote ambazo zikikutwa zina ‘reflector’ hizi, kwasababu zinafahamika kama hamjui, iwe kwenye bodaboda, iwe kwenye baiskeli, kamata na fikisha mahakamani, hatuwezi kufumbia macho uharibifu huu, utakuja kesho utakuwa wameng’oa kila kitu wataharibu. Kumbukeni kwamba bilioni 17.7 zimelala hapa, na manufaa yote mmeyasikia na ninyi mnajua zaidi, sasa mnataka kuturudisha wapi, hatutakubali uharibifu wa aina yoyote ile,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo aliyasema hayo tarehe 28.8.2019 alipotembelea daraja la Mto Momba kuona maendeleo ya daraja hilo lililojengwa na mkandarasi Jianxi Geo – Engineering (Group) Corporation kutoka China na kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia kitengo chake cha ushauri wa miradi TANROADS Engineering Consulting Unit (TECU) ambapo hadi sasa daraja hilo limeshakamilika kwa asilimia 100.
Wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa Daraja hilo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Jetrovas August alisema kuwa kazi ya nyongeza ambayo ilikuwa nje ya mkataba ni kuweka taa katika barabara ya km 1.125 ambayo ni kiunganisho cha mikoa ya Songwe na Rukwa na kuongeza kuwamiongoni mwa changamoto ni un’goaji wa ‘reflector’ katika barabara hiyo.
“Pamoja na Mkandarasi kumaliza na kukabidhi mradi kwa serikali kumeanza kujitokeza uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya barabara, moja ya uharibifu ambao tayari umeanza kujitokeza ni ung’oaji wa ‘reflector’ zilizowekwa kwenye vyuma (guardrail) vya kingo la tuta la barabara kwaajili ya kuongozea magari na vyombo vingine vya usafiri wakati wa usiku,” Alisema.
Katika Hatua nyingine, Mh. Wangabo amewapongeza wakandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri wa ya ujenzi wa barabara ya kutoka Sumbawanga – Matai – Kasanga yenye urefu wa Km 107 ambayo imefikia asilimia 91 ya ujenzina kubainisha kuwa barabara hiyo imetimiza miaka tisa tangua kuanza kwa ujenzi wake lakini pamoja na mambo mengine yaliyosababisha hayo ni maelewano mabovu yaliyokuwepo baina ya Mkandarasi na Mshauri jambo ambalo hivi sasa limemalizika na kazi inakwenda vizuri.
“Mkandarasi pamoja na ‘Consultant’ hay ani matokeo ya kuelewana, ‘Consultant’ na Mkandarasi wameelewana na wanafanya kazi usiku na mchana na matokeo yake mnayaona kazi imefanyika vizuri sana mimi nawapa pongezi sana, kwahiyo mimi nategemea kama mlivyoniambi kwenye taarifa yenu kwamba kufikia tarehe 30 mwezi Septemba barabara hii itakuwa imekwishafika bandarini kasanga na tutakuwa tumemaliza mchezo lambda marekebisho ya hapa na pale,” Alieleza.
Mradi huo wa barabara ya Sumbawanga – Matai – Kasanga unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na kugharimu Shilingi Bilioni 133.2 ambapo ujenzi wake unategemewa kumalizika mwezi Septemba mwaka 2019 chini ya Mkandarasi Joint Venture of China Railway 15G/New Century Company Ltd.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa