Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wakulima wa Mkoa huo kuhakikisha wanafuata maelekezo ya maafisa kilimo waliopo kwenye ngazi za vijiji na kata ili kuweza kulima kwa tija na hatimae kuongeza upatikanaji wa chakula katika mkoa na pia kujiongezea kipato.
Amesema kuwa ni dhamira ya mkoa kuhamasisha kilimo kinachoongeza uzalishaji kwa ekari moja, hivyo ni lazima wakulima wapande kwa kutumia utaalamu huku wakizingatia ubora wa mbegu ambazo zimehakikiwa na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu nchini (TOSC) pamoja na kutumia mbolea zinazostahili kwa ekari kama ambavyo wataalamu wanashauri
“Sio mtu anachukua mfuko mmoja wa mbolea halafu anakwenda kuuweka katika ekari mbili matokeo yake uzalishaji unakuwa ni mdogo, lakini pia baada ya mahindi kuwa yameota na kuwekewa mbolea ni lazima pia kuangalia upande wa visumbufu, wadudu wale waharibifu wa mazao, lazima tuweke dawa mapema tutumie viuatilifu ambavyo vinashauriwa na wataalamu wa kilimo, baada ya hpo tuangalie mashamba yetu kwa kupalilia kwa kufanya hivi tunaweza kuzidfi hata gunia 20 kwa ekari,” Alisema.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake maalum ya kuhamasisha kilimo chenye tija katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani humo akiwa pamoja na wataalamu wa kilimo wa mkoa na halmashauri pamoja na mkuu wa Wilaya hiyo.
Kwa upande wao mmoja wa wamiliki wa shamba lililotembelewa na Mkuu wa Mkoa Bwana Rojas Lukas amesema kuwa changamoto ubwa inayowakuta wakulima na kushindwa kuendelea kulima kilimo chenye tija ni mitaji pamoja na mdudu mharibifu aina ya kiwavi jeshi.
“Kuna mdudu Fulani anaitwa Kiwavi jeshi Yule anatusumbua sananingeomba serikali ijaribu kututafutia dawa ambayo inaweza ikamuua Yule mdudu, kingine tunaomba serikali itusaidie kama inawezekana watukopeshe ili tukuze kilimo chetu kiende mbele,” Alisema.
Akimkaribisha Mkuu wa mkoa katika shamba la mmoja wa wakulima hao mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Juliet Binyura alisema kuwa watalaamu wameendelea kutoa ushauri kwa wananchi mbalimbali na hivyo kuwaomba kuendelea kufanya hivyo ili kuwasaidia wakulima kuweza kufikia kilimo chenye tija.
“Tumekuja kuangalia utaalamu aliopewa kwa wataalamu ambao ni maafisa ugani katika kata yake na wanapanda kwa kutumia kamba na wanapima vipimo vinavyokubalika naamini ya kwamba mazao atavuna vizuri,” Alisema.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa