Wakulima wa mkoa wa Rukwa wamehimizwa kuona namna ya kujiwekeza katika kilimo cha kahawa ili kupata zao mbadala la biashara kuliko kubaki katika zao moja la mahindi ambalo mara nyingine huwa na shida ya kupanda na kushuka kwa bei kusikotabirika.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachima Wangabo alipotembelea kikundi cha watu 56 cha wakulima wa zao hilo katika Kijiji cha Katuka, Kata ya Msanzi, Wilayani Kalambo ikiwa ni miongoni mwa kuwatia moyo wakulima hao wachache ili wawe mfano kwa wakulima wengine na kuwasihi kuanzisha ushirika ili kuweza kupata soko.
Mh. Wangabo amesema kuwa kuwa kahawa huvunwa kila mwaka na kupandwa mara moja na kufanyiwa marekebisho madogo madogo pamoja na kuweza kuchanganya na baadhi ya mazao mengine ndani ya shamba moja tofauti na zao la mahindi ambalo hupandwa kila mwaka na kuongeza kuwa Serikali imejipanga kufufua zao la kahawa kwa nguvu zote.
“Changamoto ya soko serikali imeitafutia ufumbuzi, soko la kahawa litapitia kwenye Ushirika na linaenda kuuzwa kwa njia ya mnada kama inavyofanyika katika zao la korosho, kwa hali hiyo hakutakuwa na changamoto kubwa inayotarajiwa kwa zao hilo, kinachotakiwa ni kuimarisha ushirika wa kahawa” Alisema na kuongeza kuwa kama Mkoa utakuwa na Chama kikuu cha Ushirika cha kahawa.
Akisoma risala mbele ya Mh. Wangabo, Mkuu wa Idara ya kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Nicholas Mlango amesema kuwa halmashauri imeandaa kozi kwaajili ya wakulima wa kahawa na wataalamu kuendelea kuwaelimisha wakulima juu ya kujiunga na mfuko wa kahawa wataochangia ili kukuza mfuko huo.
Nae mmoja wa wakulima waliotembelewa shamba lake John Kapalata alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni kutokuwa na vifaa na elimu ya kutosha kuweza kutunza mashamba hayo ya kahawa japo wana nia ya kuendeleza kilimo hicho jambo lililopelekea Mkurugenzi wa halmashauri hiyo James Ngagani kuahidi kuwapeleka wakulima 20 wa zao hilo katika mafunzo Wilayani Mbozi na kutoa miche 30,000 bure kwa wananchi wanaohitaji kulima zao hilo.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa