Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewatoa mashaka wanarukwa juu ya kutokuwepo kwa ugonjwa wa Ebola katika Mkoa na kutahadharisha yeyote anaejaribu kuleta hofu ya ugonjwa huo katika Mkoa na kuwataka wananchi wasijengewe hofu bali waendelee kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.
Amesema kuwa Mkoa unaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya udhibiti ikiwemo kutoa taarifa na elimu kwa jamii kwa kadiri itakavyohitajika ili ugonjwa huo usiingie katika mkoa.
“Katika kipindi hiki ambacho tunatakiwa kuchukua tahadhari kubwa, wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa ni lazima tuwe na mshikamano, umoja na tahadhari kubwa sana na hasa maeneo yale ya Ziwa Tanganyika ambako kuna muingiliano wa watu kutoka Zambia, DRC, Rwanda na Burundi. Lakini pia wanaotokea maeneo mengine ya nchi, la muhimu ni kuchukua tahadhari kubwa sana,” Alisema
Ameongeza kuwa wenyeviti wa vijiji wajizatiti katika kuboresha taarifa za wakazi wao kwenye madaftari yao na kuwa makini na wageni wanaoingia kwenye maeneo yao pamoja na kuitaka idara ya uhamiaji kuhakikisha wageni wote wanaingia katika njia zilizo rasmi.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa afya Mkoa kilichoitishwa na Mganga Mkuu wa mkoa ili kutoa elimu kwa wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo waandishi wa habari juu kusambaza ujumbe huo wa kujihadhari na ugonjwa huu hatari wa Ebola.
Mmoja wa wadau hao akiwakilisha kundi la wazee, Zeno Nkoswe amesema kuwa serikali ya Mkoa haina budi kuhakikisha elimu hiyo inafikishwa kwa viongozi wote wa dini kwani wao wanauwezo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kwa muda ufupi na ujumbe hatimae kutimiza malengo ya kufisha ujumbe huo kwa wananchi.
Akichangia mjadala huo mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Rukwa, Sadrick Malila amesema kuwa serikali haina budi kutumia redio zilizopo Mkoani Rukwa ili kufikisha ujumbe huo kwa watu wote na maeneo yote ya Mkoa na mikoa ya jirani ili watu waweze kujikinga na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa Ebola upo katika nchi ya jirani ya Jamhuriya watu wa Kongo katika mji wa Biroko, jimbo la Equator na kwa taarifa za shirika la afya duniani, hadi kufikia tarehe 17 Mei, 2018 watu 44 walikuwa wamebainika kuwa na ugonjwa huo na watu 23 kufariki.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa