Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi amewataka wanasheria wa halmashauri nne za mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanazisaidia halmashauri hizo kuepukana na kesi zinazokabili halmashauri hizo mahakamani kwani halmashauri hizo zimekuwa zikiingia katika kesi nyingi huku wataalamu hao wakiwepo na kushindwa kuwashauri wakurugenzi juu ya namna ya kuepukana na kesi hizo.
Ameongeza kuwa halmashauri zimekuwa zikishindwa kesi nyingi na kupata hasara ya kulipa fedha nyingi ambazo zinegeweza kusaidia shughuli za maendeleo, hata hivyo alibainisha kuwa anafahamu juu ya changamoto za tafsiri ya sheria ndogo zilizopo ambazo muda mwingine zinalalamikiwa na wananchi na pia kuwepo kwa changamoto ya ucheleweshwaji wa utungaji wa sheria hizo.
“Nafahamu pia suala la msingi la kikao hiki ambalo ni sheria ndogo za ukusanyaji wa mapato ambavyo limekuwa na changamoto kutegemea na halmashauri husika. Mkikaa pamoja naamini kwa siku hizi mbili changamoto nyingi za eneo hili zitapata majadiliano na mapendekezo ili mkoa wetu uendelee kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato,” Alisema.
Kijazi aliyasema hayo katika ufunguzi wa kikao cha siku mbili kilichowajumuisha wataalamu wa Sekretarieti ya mkoa na wanasheria wa mamlaka za serikali za mitaa kupitia sheria ndogo ambazo zinatumika katika ukusanyaji wa mapato chini ya program ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP).
Wakati akitoa maelezo ya utangulizi juu ya kikao hicho Afisa wa Serikaloi za mitaa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alisema kuwa program hiyo ya PFMRP ya awamu ya tano (2017 -2022) ina lengo la kudhibiti na kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha za umma katika serikali na taasisi zake ili kuweza kutoa huduma bora na kuleta maendeleo endelevu.
Aidha, alisema kuwa eneo hilo linalenga kuhakikisha kwamba mamlaka za serikali za mitaa kama wadau muhimu wa utekelezaji wa bajeti, wanazingatia viwango, vigezo, taratibu, sheria na kanuni katika uendeshaji wa shughuli na utekelezaji wa majukumu yake.
“Nia ya serikali ni kuona halmashauri zote zinaongeza ukusanyaji wa mapato. Hivyo ni wazi kuwa maarifa mtakayoyapata hapa pamoja na uzoefu mtakaobadilishana utasaidia kuboresha sheria ndogo zilizopo na mwisho tuweze kuwa na sheria nzuri ambazo zikisimamiwa zitasaidia suala zima la kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani,” Alisisitiza.
Sheria ndogo zinatungwa na kusimamiwa chini ya sheria za nchi ikiwemo sheria ya serikali za mitaa sura 287 na sura ya 288, na sheria hizi zikitungwa kwa usahihi zitasaidia kusimamia ukusanyaji wa mapato, kuelewa mahitaji ya mabadiliko ya sheria kulingana na wakati, kuhimiza wananchi kulipa kodi pasi na usumbumbufu na kutenda haki kwa wananchi wa halmashauri husika.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa