Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Winnie Kijazi amewataka wataalamu wa halmashauri za mkoa huo kwa kushirikiana na wataalamu wa sekretarieti ya mkoa kuwa na mipango Madhubuti ya ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi bila kusababisha bughudhi na kero kwa walipa kodi na ushuru ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo chini ya program ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma (PFMRP V).
Amesema kuwa suala la usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ni jukumu mtambuka ambalo linapaswa kushirikisha wadau wote katika halmashauri, na kuongeza kuwa kila mkuu wa idara na kitengo anapaswa kushiriki kikamilifu kupitia sekta yake katika kuboresha suala zima la ukusanyaji wa mapato.
Wakati akieleza namna ya kukabiliana na changamoto za ukusanyaji huo alisema kuwa mamlaka hizo hazina budi kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya watumishi wasio waadilifu na wale wanaokusanya fedha bila ya kuziwasilisha benki na hivyo kusababisha “defaulters”.
“Miongoni mwa changamoto tulizonazo ni pamoja na kuwa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu ambao hawatumii POS katika kukusanya mapato na hivyo kufifisha juhudi za halmashauri za kuongeza mapato lakini pia kuwa na idadi ndogo ya POS ikilinganishwa na vituo vya kukusanyia mapato katika halmashauri,” Alisema.
Wakati akitoa neno la shukurani kwa meni rasmi wa kikao hicho mhasibu wa halmashauri ya Wilaya ya kalambo Eric Kayombo alisema kuwa kwa kupitia kikao hicho wameweza kupeana uzoefu kutokana na kushiriki kwa wataalamu wa halmashauri tofauti za mkoa huo jambo ambalo limewafanya kuona namna ya kuwa na mkakati mpya pindi watakaporudi kwenye halmashauri zao na hatimae kuimarisha mapato na kutoa huduma kwa wananchi.
Ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ndani ya halmashauri, serikali ilianzisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki (Local Government Revenue Collection Information System) LGRCIS mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo halmashauri zote nne za mkoa huo zinatumia mfumo huo huku kukiwa na mashine za kukusanyia mapato (Point of Sales Machines) POS 387 na kuongezwewa mashine nyingine 154 na OR – TAMISEMI.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa