Watumishi wa Umma wa Halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa pamoja na Sekretariet ya Mkoa wamekumbushwa wajibu wao wa kutenda haki kwa wananchi pamoja na wakuu wa idara kwa watumishi wengine ili kuboresha huduma na mahitaji ya wananchi.
Salamu hizo zizliobeba ujumbe mzito kutoka kwa Katibu Mkuu kiongozi uliwasilishwa na Waratibu wa utumishi wa umma kutoka Ofisi ya Rais Ikulu wakisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kazini na kuonya wale wanaotegea kufanya majukumu yao pamoja na wale wanaoingilia majukumu yasiyokuwa ya kwao.
Katika kusisitiza hayo wamesema kuwa ofisi ya rais Ikulu imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi, malalamiko ambayo yangeweza kutatuliwa katika ngazi ya mkoa hadi kata na hivyo kuona sababu ya kuwakumbusha watumishi wa ngazi husika kuwatumikia wananchi kwa kuwatafutia ufumbuzi wa kero zao na sio kuwakejeli na kuwadharau na matokeo yake kumwandikia rais ili aweze kutatua matatizo yao.
“Taifa letu ni zuri sana lina utawala mpaka ngazi ya chini kwa wananchi, hivyo wananchi wetu wahudumiwe, wakihudumiwa vizuri watakuwa na utulivu, amani na kutekeleza wajibu na majukumu yao na hivyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa lao, imebainika kwamba ile ngazi ambayo ipo karibu na wananchi ndiyo inayowachonganisha wananchi na serikali yao, ngazi ya kata na vijiji kwa kiwango kikubwa, ofisi zao badala ya kuwa za utumishi wa umma zimekuwa za makampuni binafsi na wao kuwa wafalme hivyo mwananchi anapokwenda pale kwaajili ya kusaidiwa anakerwa zaidi,” Alisema Francis Mangira Mratibu wa utawala wa utumishi wa Umma ofisi ya rais Ikulu.
Kwa upande wake Mratibu msaidizi wa utawala wa utumishi wa Umma ofisi ya rais Ikulu Abdalla Mlongane amesema kuwa watumishi wa umma wanapaswa kujiwekea malengo ya utekelezaji, kuyafuatiliana na kujitathmini katika utendaji wao bila ya kusahau kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ikiwemo kuheshimiana baina ya watumishi na kutunza siri za ofisi.
Nae katibu tawala msaidizi utawala na rasilimali watu Aboubakar Kunenge aliuhakikishia ujumbe huo kuwa yale yote yalioagizwa yatazingatiwa na kufanyiwa kazi na hivyo watumai matokeo mazuri kutoka kwa watumishi waliopo katika mkoa wa Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa