Watumishi wa sekta ya afya mkoani Rukwa wamehimizwa kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.

Wito huo umetolewa leo tarehe 17 Desemba 2025, katika kikao cha Mfuko wa Bima ya Taifa kilichowakutanisha wataalamu wa afya kutoka vituo mbalimbali vya kutolea huduma mkoani humo.Kikao hicho kililenga kujadili namna bora ya kuimarisha utekelezaji wa mpango huo ngazi ya jamii.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Katibu Tawala wa Mkoa,Ndugu Robert Msalika Makungu, amesema kuwa uelewa wa wananchi kuhusu Bima ya Afya kwa Wote ni jambo la msingi katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kutoa huduma za afya zilizo nafuu, endelevu na zinazopatikana kwa wakati.
Ameeleza kuwa wananchi wengi hukumbwa na changamoto ya kugharamia huduma za afya pindi wanapopatwa na magonjwa ya ghafla au dharura,hali inayoweza kusababisha kuchelewa au kushindwa kabisa kupata matibabu stahiki.Kupitia Bima ya Afya kwa Wote,wananchi wataweza kupata huduma muhimu za afya bila kulazimika kubeba mzigo mkubwa wa kifedha wakati wa uhitaji. “Watumishi wa afya mna nafasi ya kipekee ya kuwafikia wananchi moja kwa moja.Elimu mnayotoa siyo tu kuhusu matibabu, bali pia kuhusu kinga na maandalizi ya kifedha kwa afya zao,”amesema Ndugu Msalika.
Amehimiza matumizi ya njia jumuishi za mawasiliano ikiwemo mikutano ya hadhara,vikao vya kijamii, nyumba za ibada na majukwaa ya mitandao ya kijamii ili ujumbe kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya uwafikie wananchi wengi zaidi kwa lugha rahisi na inayoeleweka.

Aidha,amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kaya maskini zinatambuliwa kwa haki na usahihi ili ziweze kunufaika na mpango wa kulipiwa bima ya afya, hatua inayolenga kulinda utu wa mwananchi na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika kupata huduma za afya. Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msisitizo kwamba elimu ya bima ya afya si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa pamoja unaohitaji ushiriki wa jamii.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa