Mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Zambia Mhe. Bernard Mpundu ameambatana na viongozi wengine kutoka nchini Zambia katika kushiriki Kongamano la Uwekezaji Mkoni Rukwa.
Awali Mhe. Mpundu alitembelea katika mabanda ya maonesho ya bidhaa katika viwanja vya Nelson Mandela na baadae katika Bandari ya Kabwe na Kipili kuweza kujionea miundombinu ya bandari hizo.
Baada ya kutembelea na kujionea bandari hizo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uwekezaji mkubwa wa bandari zenye kiwango cha Kimataifa Mkoani Rukwa tofauti na nchini Zambia.
Aidha ameipongeza Serikali kwa kutumia wakandarasi wazawa katika ujenzi wa bandari hizo na kuwa ujenzi huo unasaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali katika kukamilisha miradi mikubwa kama bandari.
Mhe. Mpundu ametoa wito kwa makampuni mbalimbali kutoka Zambia kuja kuwekeza kwenye bandari hizo kwa kujenga meli au boti kubwa za kusafirisha mizigo na abiria kutokana na mahitaji makubwa ya wananchi kutumia vyombo vya maji kwa wingi katika maeneo ya Kabwe na Kipili.
Kongamano la uwekezaji Mkoani Rukwa limewakutanisha wafanyabiashara kutoka Sehemu mbalimbali zikiwemo ndani na nje ya nchi lengo likiwa ni kutazama na kutangaza fursa za uwekezaji Mkoani Rukwa. Kongamano hilo lililoanza mnamo Mei 25 2023 linatarajiwa kuhitimishwa Mei 30 2023.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa