Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbwanga Dk. Khalfan Haule kuhakikisha anatafuta dawa ya kuulia panya wakiwa mashambani ili kuokoa miti kutokana na uchomaji wa misitu kwasababu ya uwindaji wa panya.
Amesema kuwa ameisikia changamoto hiyo ya uchomaji wa misitu kwasababu ya uwindaji wa panya kutoka kwa vijana mbalimbali wanaojishughulisha na mashamba ya upandaji miti pamoja na taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga juu ya changamoto za kuendeleza misitu.
“DC tafuta dawa ya panya, wauliwe huko mashambani, ili panya wasiwepo na miti iokoke, mbona hamshangilii? Hawa panya tutawaua kwa sumu huko mashambani wasiwe chanzo cha mioto ambayo mnachoma huko kuwatafuta hawa panya ili wafie huko huko mashimoni msiwapate,” Alisisitiza.
Agizo hilo amelitoa katika muendelezo wa kampeni ya upandaji miti mijini na vijijini katika Kijiji cha Mpwapwa, kata ya Mpwapwa, Wilayani Sumbwanga baada ya kuwauliza wananchi wa Kijiji hicho juu ya changamoto aliyoisikia ya uchomaji wa moto misitu kutokana na kuwinda panya, japo wananchi walikataa.
Pia katika kuongezea hilo alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuhakikisha anasimamia sheria ya hifadhi ya mazingira na kuwawajibisha wote wanaohusika na uharibifu wa mazingira.
Nae akisoma taarifa Mkurugenzi wa H/W ya Sumbawanga Nyangi Msemakweli alibainisha kuwa miongoni mwa changamoto ni muitikio mdogo wa uhifadhi wa mazingira pamoja na mila na tamaduni za wananchi za uwindaji wa panya hali inayosababisha uchomaji wa misitu wakati wa kiangazi.
“Changamoto nyingine ni baadhi ya viongozi wa serikali ya Kijiji kujihusisha na uuzajia wa maeneo yaliyotengwa kwaajili ya hifadhi ya Kijiji na usimamizi mdogo wa sheria ndogo za vijiji katika utunzaji wa misitu,” Alimalizia.
Mmoja wa vijana wanaojishughulisha na upandaji kiti wa kibiashara Julius Magaga alimweleza Mh. Wangabo kuwa chnagmoto inayowakatisha tamaa vijana wengi ni kutokana na uwindaji wa panya uliokithiri na kusababisha hasara katika misitu.
Kwa msimu wa 2017/2018 hadi 30/1/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Sumbwanga imepanda miti 830,527 ambayo ni sawa na 55.4% na ina misitu 92 yenye ukubwa wa jumla ya Hekta 49,179.6. Huku Mh. Wangabo akigawa miche 850 kwa kaya 850 za Kijiji cha Mpwapwa, Wilayani Sumbawanga.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa