Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Rukwa
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maghala na vihenge vya kisasa kanda ya Sumbawanga kuongeza kasi ili kukamilisha haraka mradi huo kwa mujibu wa makubaliano.
Alisema kuwa kampuni iliyoteuliwa baada ya kushinda zabuni kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ni UNIA ARAJ REALICZJE ya nchini Poland ambayo ilimteua mkandarasi msaidizi mzawa anayejulikana kwa jina la ELERAI CONSTRUTION CO. LTD wa Arusha, hivyo napaswa kuongeza kasi ya ujenzi kutokana na kasi iliyopo kwa sasa kutoridhisha.
Waziri Hasunga ameyasema hayo juzi tarehe 10 Octoba 2019 mara baada ya kutembelea ujenzi wa mradi huo kwenye Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi utakaowanufaisha wakulima wa mazao ya nafaka kwani serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko (CPB) itakuwa na uwezo wa kununua mazao mengi kwa wakulima na kuyahifadhi kwa muda mrefu.
Alisema kuwa kampuni hiyo inayojenga vihenge vya kisasa na miundombinu mingine ikiwemo maghala katika eneo la Kanondo Manispaa ya sumbawanga mkoani Rukwa na Mpanda Mkoani Katavi bado haijamfurahisha kutokana na kasi ndogo ya ujenzi wa mradi.
Mhe Hasunga amesema kuwa serikali imekusudia kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka nchini ili kuwanufaisha wakulima punde wanapovuna mazao yao hususani nafaka kwani kufanya hivyo wakulima wataongeza uzalishaji na tija kwenye mazao na kuliongezea Taifa pato kubwa.
Alisema kuwa vihenge hivyo vitakuwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya Tani 20,000 za nafaka huku ujenzi wa miundombinu mingine ukiendelea kama jingo la Ofisi ya utawala, Ghala la kawaida la ujazo wa Tani 5000 za nafaka, na Mzani mkubwa wa daraja (Electronic weighbridge).
Mradi huo utakuwa na gharama ya Dola za kimarekani 6,019,399 ambazo ni takribani shilingi za Kitanzania Bilioni 14 kwa mradi wa eneo la Kanondo Sumbawanga na vilevile Dola za Kimarekani 6,180,857 sawa na fedha za kitanzania Shilingi Bilioni 14.2
Mhe Hasunga ametilia nyundo kuwa serikali haitaongeza muda kwa mkandarasi endapo atashindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Muda wa mradi kuanza hadi kukamilika ni jumla ya miezi 18 (Mwaka mmoja na nusu), Kwa upande wa Mpanda mkoani Rukwa mradi umeanza tarehe 14 Januari 2019 na umepangwa kukamilika tarehe 14 Julai 2020 wakati upande wa Kanondo mkoani Katavi mradi huo umeanza tarehe 8 Septemba 2019 na unatarajiwa kukamilika tarehe 8 Machi 2021.
Punde mradi huu utakapokamilika mkoa wa Rukwa utakuwa na Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) yenye uwezo wa kuhifadhi nafaka za Tani 58,500 wakati mkoa wa Katavi utakuwa na uwezo wa kuhifadhi Tani 28,000 ikihusisha pia maghala ya zamani.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa