Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS kuchangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mponda katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ametoa agizo hilo kufuatia taarifa iliyowasilishwa kwake na Mtendaji wa Kata ya Majengo, Matage Bikaniko Mjarifu alipotembelea kijiji hicho kinachopakana na Msitu wa Mbizi ambapo amesema wananchi wa kijiji hicho husafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 11 kwa ajili ya kufuata huduma za afya mjini Sumbawanga.
Amesema mpaka sasa wananchi wa kijiji hicho wameshachangia shilingi laki 9 na Mbunge wa Sumbawanga mjini shlingi milioni 5. Hata hivyo amesema jumla ya shilingi milioni 134 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Kigwangalla alisema Wizara yake kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS itachangia shilingi Milioni 20, hivyo wananchi wapambane kwa kushirikiana na halmashauri yao ili jengo hilo lisimame na hatimaye fedha hizo ziwasilishwe kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wake.
Alisema Falsafa ya Uhifadhi Endelevu ni Uhifadhi Shirikishi Jamii, hivyo wizara yake itaendelea kusimamia sera ya kuhakikisha wananchi hususan wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi wananufaika moja kwa moja na hifadhi hizo kupitia miradi ya maendeleo.
Dk. Kigwangalla ameziagiza taasisi zote za uhifadhi nchini kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya jamii ili wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hizo waone umuhimu wa hifadhi hizo moja kwa moja na hivyo kutoa ushirikiano kwenye uhifadhi.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa