MAJALIWA : HALMASHAURI TUMIENI FEDHA ZA NDANI KUKAMILISHA MIRADI
Na. OMM Rukwa
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Rukwa ambapo ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Paramawe na hospitali ya Wilaya iliyopo Wilayani ya Nkasi.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Paramawe leo (Desemba 14,2022) inayojengwa kupitia mradi wa SEQUIP ambapo ameweka jiwe la msingi la mradi huo uliogharimu Shilingi Milioni 470 kujenga vyumba nane vya madarasa,maabara,maktaba na matundu ya vyoo.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi huo, Waziri Mkuu amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Rashid Mchatta kumsimamia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi William Mwakalambile ili ahakikishe anakamilisha maeneo ya ujenzi wa shule hiyo kwa kutumia mapato ya ndani.
“Milioni 470 zimetumika na mmetumia zingine za halmashauri lakini miundombinu bado. Nataka shule hii ikamilike na Januari 2023 wanafunzi waingie” Alisema Majaliwa
Kuhusu ujenzi wa hospitali ya Wilaya Nkasi, Waziri Mkuu aliewaeleza wananchi kuwa serikali itaendelea kukamilisha miradi yote ya afya ikiwemo kuhahikisha vifaa tiba vinapatikana kwa ajili ya wananchi kupata huduma.
Aidha, Waziri Mkuu amemwagiza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi -Afya kukutana na uongozi wa halmashauri ya Nkasi ili kujua kwanini mradi ya ujenzi wa majengo saba ya hospitali ya wilaya haujaanza wakati tayari fedha zilikwishatolewa na serikali.
“Naibu Katibu Mkuu Tamisemi urudi hapa Nkasi kesho kufuatilia kwanini majengo saba hayajaanza wakati fedha ipo” aliagiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika hatua nyingine Majaliwa ameagiza Mkuu wa Mkoa huo na Katibu Tawala wa Mkoa kuitisha kikao cha mawakala wa mbolea mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha wakulima wanapata pemebejeo hiyo muhimu kwa kuwa serikali imekwisha toa fedha za ruzuku .
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alisema mkoa unaendelea na usimamizi wa shughuli za maendeleo na kuwa wananchi watapata huduma stahiki.
Waziri Mkuu kesho ataendelea na ziara yake kwenye wilaya za Kalambo na Sumbawanga.
Mwisho.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa