Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameagiza kukamatwa kwa mhandisi wa ujenzi Ding Fubing pamoja na mshauri elekezi wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Rukwa Swalehe Kyabega kutokana na kushindwa kukamilisha mradi huo kwa wakati huku wakiendelea kusuasua juu ya ukamilifu wa ujenzi huo ambao ulitakiwa kukamilika 30.12.2019 baada ya kuongezewa siku 100 na hatimae hadi sasa wamefikia asilimia 52 ya ujenzi.
Prof. Ndalichako alisema kuwa kimkataba mkandarasi huyo alitakiwa kuthibitisha kwa risiti matumizi ya shilingi bilioni 1.5 malipo ya awali ya ujenzi kupitia kwa Mshauri elekezi ambae alishindwa kutoa vielelezo vinavyoonesha utekelezaji wa takwa hilo la kisheria na kuongeza kuwa mshauri huyo ameshindwa kusimamia matumizi ya fedha za serikali katika utekelezaji wa mradi huo.
“Mkandarasi aende akakae ndani mpaka vile vifaa mlivyoruhusu viondoke hapa, mpaka vitakaporudi ndio muwaachie, wasababu naona sasa hii inakuwa ni kuchezeana, majibu hamna kitu ambacho kinachoeleweka, utakwenda kukaa sero hadi utakapotoa maelezo ya ufasaha juu ya jambo hili, kwasababu huwezi kucheza na serikali namna hii, mara ya mwisho nilipokja hapa mlikuwa na vifaa kama vyuma chakavu, mmeleta vifaa ahalafu mmeviondoa kuvuipeleka sehemu nyingine, utakaa ndani hadi vifaa hivyo vitakaporudi na uwe na watu wa kutosha kufanya kazi, kwasababu tumechoka tunataka huu ujenzi uishe, wachukue wakae ndani,” Alisisitiza.
Halikadhalika mhandisi huyo alionekana kuwafanyika kazi wafanyakazi wa mradi huo kwa malipo ambayo yapo kinyume na mkataba wa serikali huku baadhi ya watendaji wengine wa sekata ya umeme wakilalamika kufanyishwa kazi bila ya mkataba maalum.
Prof. Ndalichako aliyasema alipotembelea ujenzi wa chuo cha ufundi Stadi VETA katika eneo hilo la Kashai lililopo Manispaa ya Sumbawanga huku akiongozana na watumishi idara ya elimu kutoka halmashauri mbili za wilaya ya Sumbawanga, Mkuu wa Wilaya hiyo, kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na uongozi wa VETA taifa.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho Mkurugenzi Mkuu wa VETA nchini Dkt.Pancras Bujuru alisema kuwa mkandarasi huyo tayari amelipwa shilingi 3,507,174,603 ambayo ni sawa na asilimi 35 ya thamani ya mradi huo na malipo ya mwisho yalikuwa shilingi 330,521,213.79 ambapo alilipwa tarehe 20.12.2019 na kutegemea kuwa baada ya malipo hayo kasi ya ujenzi ingeongezeka lakini haikuwa kama walivyotaraji.
Mh. Waziri kwa hali hii mkandarasi amethibitisha uwezo mdogo kutekeleza mradi huu na hatuna imani kama utatekelezwa kwa wakati kwasababu muda aliopewa na kuongezewa siku 100 vyote vimekwisha nab ado kazi hazijaweza kuisha kwa muda, kwahiyo tunadhani kwamba uwezo wake wa kutekeleza mradi hauturidhishi hata sisi, mshauri elekezi anajukumu la kumsimamia mkandarasi kwa niaba yetu kwasababu tumemuajiri kwa kazi hiyo, tunajua kwamba amekuwa akitoa maelekezo lakini kumekuwa na udhaifu wa kuyasimamia kwa kuchukua hatua zinazostahili na kwa muda muafaka naye tunadhani ana mapungufu,” alisema.
Tarehe 31/8/2019 mkandarasi Tender International alikabidhiwa kiwanja kwaajili ya kuanza ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Manispaa ya Sumbawanga pamoja mshauri Elekezi wa Mradi huo Sky Architect Consultancy Ltd, ambapo mradi huo ulitegemewa kukamillika mwezi Septemba 2019 huku gharama za mradi huo ikiwa shilingi 10,700,488,940.05.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa