Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb) amefanya uzinduzi wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 1.8 katika Wilaya ya Kalambo Mkoa wa Rukwa leo Oktoba 1, 2024.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku tatu Mkoani hapa, Mheshimiwa Chana amezindua mradi wa Maji wa Kilewani wenye thamani ya shilingi milioni 597.6. Mradi wa maji wa Kilewani ni miongoni mwa miradi ya maji iliyojengwa kwa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (National Water Fund) na unahudumia wakazi wapatao 3, 847. Mradi huo umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake.
Miradi mingine iliyozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Chana ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Josephat Kandenge iliyoko Kata ya Mpombwe, mradi uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 583.1 hadi kukamilika kwake.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Chana amezindua pia mradi wa ujenzi wa Shule mpya ya Msingi ya Namlangwa iliyoko Kata ya Lyowa wenye thamani ya shilingi milioni 638.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kalambo, Mheshimiwa Waziri Chana amesema Serikali imedhamiria kutatua changamoto ya umbali wa upatikanaji wa huduma kwa kuhakikisha inasogeza huduma za maji, elimu na afya karibu zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Pindi Chana amewataka wananchi kutunza miradi inayojengwa na Serikali ili azma ya huduma kusogezwa karibu na wananchi itimie. Ameeleza kuwa upatikanaji wa maji, elimu na afya karibu na makazi ya wananchi utaongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kuongeza kipato cha wananchi.
Wananchi Wilayani Kalambo wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Chana yuko ziarani Mkoani Rukwa, ziara itakayochukua siku 3.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa