Wito umetolewa kwa wazazi na walezi Mkoani Rukwa kuhakikisha kila mtoto aliye na umri wa chini ya miaka nane anapatiwa chanjo ya Polio ili kumkinga na ugonjwa wa huo.
Wito huo umetolewa na Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere Mkuu wa Mkoa wa Rukwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya chanjo uliofanyika leo Septemba 21, 2023 katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua Manispaa ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa. Mheshimiwa Makongoro alimwakilisha Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb) Waziri wa Afya.
Ametoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote za Mikoa ya Kagera, Kigoma Katavi Rukwa , Songwe na Mbeya kupitia Kamati za Afya ya Msingi za Mikoa na Halmashauri (PHC) kusimamia Kampeni hii na kuhakikisha wanamfikia kila mtoto aliyelengwa kupatiwa chanjo mahali popote alipo.
Amezitaka taasisi za umma na binafsi, viongozi wa dini, asasi za kiraia, wawakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii na vyombo vya habari kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI katika kuhakikisha kuwa kampeni hiyo inafanikiwa.
Amewataka pia wananchi kutoa ushirikiano kwa timu za watoa huduma katika maeneo yote ili watoto waliolengwa waweze kupatiwa chanjo.
Mheshimiwa Charles Makongoro Nyerere ameyashukuru mashirika ya Kimataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), UNICEF na Save the Children kwa Ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kutokomeza Polio
Jumla ya watoto 391,883 wanatarajiwa kupatiwa chanjo Mkoani Rukwa.
Hakimiliki © 2017 Mkoa wa Rukwa. Haki Zote Zimehifadhiwa